*Dodoma*
Wilaya ya Nanyumbu, mkoani Mtwara, imeanza kunufaika na rasilimali zake za madini baada ya Serikali kuthibitisha kuwa madini ya dhahabu yenye thamani ya shilingi bilioni 1.28 yamezalishwa wilayani humo katika kipindi cha miaka minne (2020–2023).
Hayo yameelezwa leo Mei 20 2025 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nanyumbu, Mhe. Ally Yahya Mhata, aliyetaka kufahamu mapato yaliyopatikana kutokana na shughuli za madini wilayani humo kati ya mwaka 2021 hadi 2023.
Dkt. Kiruswa ameeleza kuwa, kupitia mauzo ya madini hayo, Serikali imekusanya jumla ya shilingi milioni 93.33 kutoka kwenye vyanzo mbalimbali ikiwemo mrabaha, ada ya ukaguzi pamoja na ushuru wa huduma (service levy) unaolipwa kwa Halmashauri.
“Wilaya ya Nanyumbu ina jumla ya leseni za uchimbaji mdogo wa madini 66 ambazo bado zipo hai. Tunawahimiza wamiliki wa leseni hizo kuendeleza maeneo yao na pia kuwakaribisha wadau wengine wenye nia na sifa kujisajili rasmi ili kushiriki katika maendeleo ya sekta hii muhimu,” alisema Dkt. Kiruswa.
Aidha, Dkt. Kiruswa amesisitiza kuwa, Wizara ya Madini inaendelea kutoa elimu na hamasa kwa wachimbaji ili kuongeza uzalishaji na hatimaye kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Wilaya ya Nanyumbu na mkoa wa Mtwara kwa ujumla.
Aidha, akizungumzia ahadi ya Serikali kugawa vitalu vya uchimbaji wa madini kwa wachimbaji wadogo, Dkt. Kiruswa amesema kuwa, hivisasa mkakati wa Wizara ya Madini ni kufanya utafiti wa kina ili kubaini maeneo yote yenye rasilimali madini na aina za madini hayo, hivyo Serikali itatenga maeneo hayo baada ya kupata uhakika wa maeneo yenye madini ili wachimbaji hao wasichimbe kwa kubahatisha tena badala yake wachimbe kwa tija zaidi.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na rasilimali za madini kwa njia endelevu, shirikishi na yenye tija kwa taifa.