Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
Dar es Salaam, Mei 21 – KATIKA juhudi za kujenga jamii yenye usawa na haki, Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam, kupitia Kituo chake cha Tegeta, kimetoa mafunzo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza hadi wa tatu kuhusu usawa wa kijinsia kupitia mradi wa HEET (Higher Education for Economic Transformation).
Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha wanafunzi kutambua haki zao, kupinga ukatili wa kijinsia na kuondoa mila kandamizi zinazoendeleza ubaguzi wa kijinsia katika jamii.
Mkuu wa Chuo, Prof. Cyriacus Binamungu, amesema kuwa Mzumbe imejikita katika kutoa elimu ya usawa wa kijinsia kwa vitendo, sambamba na sera na sheria zilizoandaliwa na chuo hicho kwa mujibu wa mikataba ya kikanda na kimataifa iliyoridhiwa na Tanzania.
“Mafunzo haya yanasaidia kuwaondolea vijana wetu dhana potofu wanazozikuta katika jamii zao kuhusu nafasi ya mwanamke na mwanaume,” alieleza Prof. Binamungu.
Mkurugenzi wa Chama cha Waelimishaji wa Masuala ya Usawa wa Kijinsia Afrika, Bi. Neema Kitundu, alisisitiza umuhimu wa kuheshimiana miongoni mwa wanafunzi. Alisema hakuna jinsia iliyo bora zaidi ya nyingine na akaeleza kuwa ukatili wa kijinsia upo katika aina mbalimbali kama vile kiuchumi, kimwili na wa kimiundombinu.
Kutoka upande wa mradi wa HEET, Dkt. Perpetua Kalimasi alibainisha kuwa elimu hiyo tayari imetolewa kwa shule za sekondari na jamii zilizo jirani na Mzumbe. Alisema elimu ya kijinsia si tu kwa wanachuo bali ni kwa jamii nzima ili kusaidia kupunguza vitendo vya ukatili.
“Mafunzo haya yanachangia kujenga kizazi kinachotambua thamani ya usawa, haki na utu wa binadamu,” alisema Dkt. Kalimasi, akibainisha kuwa juhudi hizo zitaendelea kufikia matawi mengine ya chuo.
Kwa upande wake, Dkt. Moses Ndunguru alieleza kuwa wanafunzi 810 tayari wameshapata mafunzo hayo. Alionya kuwa ukatili wa kijinsia ni hatari kwani huweza kuvunja haki za binadamu na kudhalilisha utu wa mtu.
Mafunzo haya yamekuwa sehemu ya mkakati mpana wa Chuo Kikuu Mzumbe katika kuandaa wahitimu wanaotambua wajibu wao katika kujenga jamii jumuishi na yenye usawa wa kijinsia.


Matukio mbalimbali.