Bidhaa zilizoteketezwa leo na TBS katika dampo la Chidaya Jijini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeteketeza bidhaa za chakula na vipodozi zilizoisha muda wa matumizi tani mbili zenye thamani ya shilingi milioni 32.7 zilizokamatwa kutoka kwenye maeneo ya biashara katika Mikoa ya Dodoma, Singida Na Tabora.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 23,2025 mara baada ya kuteketeza bidhaa hizo katika dampo la Chidaya Jijini Dodoma, Afisa Mkaguzi wa TBS Bw. Magesa Mwizarubi ambapo amesema kuwa zoezi hilo limefanyika katika kipindi cha mwezi Disemba 2024 hadi Mei 2025.
“Zoezi hili la uteketezaji wa bidhaa ambazo hazina ubora zina jumuisha bidhaa za vyakula ambazo zimeisha muda wake wa matumizi, bidhaa za vipodozi zenye viambatanishi sumu,bidhaa zilizo haririwa tarehe za mwisho wa matumizi pamoja na bidhaa ambazo hazijasajiliwa nchini,bidhaa hizi zinauzito wa tani mbili zenye thamani ya milioni 32,761,300/-.
Bw. Mwizarubi amesema bidhaa hizo zilizoteketezwa kama zingeendelea kutumika zingeli sababisha Athari kubwa kiafya kwa watumiaji na uchumi wa Taifa kiujumla.
“Bidhaa hizi ni matokeo ya kaguzi ambazo zimefanywa katika maeneo ya biashara ya Halmashauri zote za mikoa ya Dodoma,Singida na Tabora hizi bidhaa zina madhara na Athari za kiafya kwa watumiaji,kwa upande bidhaa za vyakula zilizoisha muda wa matumizi athari zake ni za muda mfupi na muda mrefu pamoja na Saratani,upande wa vipodozi zina madhara na athari za muda mfupi za kiafya kama kuathiri ngozi,macho na mfumo wa uzazi kwa wanawake,”amesema.
Aidha amesema shirika hilo litaendelea na ukaguzi katika maeneo ya biashara nchi nzima huku likiwataka wafanyabiashara hao kuhakikisha wanakuwa na utamaduni wa kukagua bidhaa za vyakula na vipodozi ili kujilizisha ubora wake na kuacha mara moja kuuza bidhaa zilizoisha muda wa matumizi huku akisema kuwa atakaye bainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Afisa Mkaguzi wa TBS Bw. Magesa Mwizarubi, akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuteketeza bidhaa hizo katika dampo la Chidaya Jijini Dodoma.
Trekta likiteketeza bidhaa za chakula na vipodozi vilivyoisha muda wake, katika dampo la Chidaya Jijini Dodoma.
Bidhaa zilizoteketezwa leo na TBS katika dampo la Chidaya Jijini Dodoma.