Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Ally Possi akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 28, 2025 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam.
……….
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inatarajia kuendesha mafunzo kwa Mawakili wote wa Serikali kutoka kwenye Wizara, taasisi za Serikali, mashirika ya umma, Ofisi za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa waliopo nchi nzima kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Mafunzo hayo yatafanyika kuanzia tarehe 02 Juni, 2025 hadi tarehe 04 Juni, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa AICC, jijini Arusha.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Dkt. Ally Possi, Wakili Mkuu wa Serikali kwa waandishi wa habari wakati akizungumza nao leo kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam. Dkt. Possi amewaeleza kuwa Kauli mbiu ya mafunzo hayo kwa mwaka huu ni: “Ubobezi wa Kisheria kwa Ajili ya Kesho: Teknolojia, Mikakati na Mizania Binafsi kwa Mawakili wa Serikali katika Kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050”.
Kauli mbiu hii inaakisi mafunzo yatakayotolewa kwa Mawakili wa Serikali kwa kuwa imezingatia nafasi na majukumu ya Mawakili wa Serikali na tasnia ya sheria kwa ujumla kama nguzo ya maendeleo ya taifa letu kama ilivyoainishwa kwenye moja ya nguzo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayohusu Uchumi Imara, Jumuishi na Shindani inayolenga nchi yetu kufikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2050.
Dkt. Possi ameongeza kuwa “Hatuna budi kutoa mafunzo ya kimkakati kwa Mawakili wa Serikali ili waendane na mabadiliko mbalimbali katika Sekta ya Sheria ili wanasheria wa Serikali waweze kuwa na utaalam ambao utaboresha uwezo wao wa kitaaluma kuendana na maendeleo ya sasa duniani,” amefafanua Dkt. Possi.
Mafunzo ya mwaka huu yatajikita kwenye mada mbalimbali zitakazogusa mbinu za kisasa na ujuzi wa mifumo ya kisheria utakaoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kupitia mafunzo hayo, Mawakili wa Serikali watapata nafasi ya kipekee ya kujifunza kutoka kwa wataalamu wabobezi wa ndani na nje ya nchi katika sekta mbalimbali ikiwemo sheria, teknolojia, uongozi na masuala ya kitaifa na kimataifa.
Mawakili watafundishwa mada mbalimbali zikiwemo:-Uelewa wa namna bora ya kuendesha majadiliano ili kufikia suluhu nje ya vyombo vya sheria;Uelewa mpana wa sheria za uwekezaji;Uelewa wa fidia na madai ya uvunjaji wa mikataba;
Sheria ya Masoko ya Mitaji Tanzania na nafasi ya Mamlaka na Baraza la Masoko la Mitaji katika utatuzi wa Migogoro; naUsimamizi bora wa mikataba ya miradi ya ujenzi.
Vile vile Dkt. Possi amesema kuwa kupitia mafunzo hayo, Mawakili wa Serikali watajifunza mbinu za kisasa zitakazowawezesha kufanya kazi kwa tija zaidi kwa kutumia teknolojia; watapata maarifa na uwezo wa ziada wa kutoa huduma za kisheria kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia mabadiliko ya kisheria na ya kijamii yanayoendelea kujitokeza.
Hivyo, Mawakili wa Serikali watakuwa na nafasi nzuri ya kutoa ushauri wa kisheria kwa Serikali na kuitetea katika vyombo vya sheria kuendana na karne ya 21 na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Vilevile, Dkt. Possi amesema kuwa Ofisi yake imeendelea kuboresha na kuunda mifumo mbalimbali ya kieletroniki inayotumika kwa shughuli za Ofisi ili kuendana na mpango wa Taifa katika matumizi ya TEHAMA ambapo Ofisi itazindua Mfumo wa Menejimenti ya Taarifa za Mashauri (Case Management Information System – CIMS) ambao unasajili mashauri yanayopokelewa na Ofisi, kuhifadhi taarifa mbalimbali za mashauri, takwimu na aina za mashauri yanayoendeshwa kwa kipindi husika.
Pia, kutakuwa na uzinduzi wa tovuti na Maktaba Mtandao (Website & e-Library) na Mwongozo wa Chapa ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OSG Branding Manual).
Dkt. Possi ametoa rai na kuwaalika Mawakili wa Serikali kushiriki mafunzo hayo muhimu yatakayofanyika kuanzia tarehe 2 mpaka 4 Juni, 2025 ambayo yatafunguliwa rasmi na Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb), Waziri wa Katiba na Sheria.
Prisca J. Ulomi
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini