Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka Waislamu kuzingatia mafunzo yanayotokana na ibada ya Hijja, hususan utii kwa Mwenyezi Mungu, mshikamano, na maadili bora ya kijamii katika kuilinda amani ya dini ya Kiislamu.
Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika Baraza la Eid lililofanyika leo, tarehe 10 Juni 2025, katika ukumbi wa Dkt. Ali Mohammed Shein – SUZA, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.
Aidha, amesema kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuwawezesha wananchi wengi zaidi kutekeleza ibada hiyo muhimu, ikiwemo kuharakisha uanzishwaji wa Mfuko wa Hijja, pamoja na kuwezesha safari za moja kwa moja za ndege kutoka Zanzibar hadi Saudi Arabia.
Vile vile, amewaomba viongozi wa dini na wananchi wote kuiombea Zanzibar iendelee kuwa na amani kabla na baada ya uchaguzi mkuu kwa kueleza kuwa mazingira ya utulivu ni nguzo muhimu ya kuimarisha maendeleo ya jamii.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi ametumia fursa hiyo kutoa salamu za Sikukuu kwa wananchi wote wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla, huku akitoa pongezi kwa Kamati ya Maandalizi ya Baraza hilo, Jeshi la Polisi kwa gwaride la heshima, pamoja na vyombo vya habari kwa kufanikisha utoaji wa taarifa kwa umma.
Kwa upande mwingine Alhaj Dkt. Mwinyi amehitimisha hotuba yake kwa kuwaombea mahujaji wote walioko Makka warejee nyumbani salama, sambamba na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu wagonjwa na wale waliotangulia mbele ya haki.
Baraza hilo limehudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman; Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla; Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi; pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, Dini, na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.