…………….
Na Sixmund Begashe, Katavi
Maofisa na Askari wapya wa Jeshi la Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wametakiwa kusimamia ipasavyo majukumu ya uhifadhi katika maeneo watakayopangiwa ili kuimarisha ulinzi wa rasilimali za taifa na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba alipokuwa akifunga mafunzo ya Maofisa na Askari hao 238 katika Kituo cha Mafunzo Mlele, mkoani Katavi.
CP. Wakulyamba amesisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kulinda mazingira na rasilimali za taifa na kuwasihi kujenga mshikamano, nidhamu na maadili mema katika utendaji wao wa kazi.
“Hakikisheni mnakuwa waadilifu, watiifu na wanyenyekevu katika utekelezaji wa amri halali kutoka kwa viongozi wenu na kamwe msijihusishe na vitendo vya rushwa,”amesema.
Ameongeza kuwa “Jeshi la Uhifadhi halitavumilia askari au Ofisa yeyote atakayehujumu juhudi za uhifadhi kwa kupokea rushwa au kuruhusu shughuli haramu kama uingizaji wa mifugo na uchimbaji wa madini ndani ya hifadhi.”
Naibu Katibu Mkuu huyo amewapongeza Askari na Maofisa wote waliomaliza mafunzo hayo kwa mafanikio na kuwashukuru wakufunzi waliojitolea kuhakikisha mafunzo ya miezi sita yanafanikishwa kwa ubora unaotakiwa.
Mafunzo hayo ni sehemu ya maboresho ya utendaji katika Jeshi la Uhifadhi la TANAPA na wahitimu 238 waliohitimu kati yao, 229 ni Askari waliopitia kozi ya awali ya Jeshi la Uhifadhi, watatu wamehitimu kozi ya mabadiliko ya muundo wa utendaji kazi na sita wamehitimu kozi ya Uongozi kwa Askari Uhifadhi waliopandishwa vyeo kuwa Maofisa.