Na Silivia Amandius.
Missenyi, Kagera.
Mbunge wa Jimbo la Missenyi mkoani Kagera, Mhe. Frolent Kyombo, anatarajia kuanza ziara ya siku nane kuanzia Juni 16 hadi 19, 2025, kwa lengo la kufanya tathmini ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa chini ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Ziara hiyo itamfikisha katika kata zote 20 za jimbo hilo, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uwajibikaji na kutoa mrejesho kwa wananchi kuhusu hatua zilizopigwa katika kipindi cha uongozi wa awamu ya sita.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mhe. Kyombo alisema kuwa ziara hiyo inalenga kusogeza huduma kwa wananchi na kuwapa fursa ya kushiriki kikamilifu katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
“Nitakwenda moja kwa moja katika kila kata kusoma utekelezaji wa ilani. Hii ni hatua muhimu kwa sababu zamani tulikuwa tukifanya hivyo ndani ya ukumbi wa wilaya mara moja, lakini sasa tuna zaidi ya wajumbe 6,000 walioko ndani ya kata,” alisema.
Alieleza kuwa si rahisi kuwakutanisha wajumbe wote hao sehemu moja, hivyo ni lazima kuwatembelea katika maeneo yao ili kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo barabara, shule, na madarasa yaliyojengwa katika kipindi cha miaka mitano ya serikali ya sasa.
“Mimi kama mbunge, nikiulizwa, nataka niweze kusema kwa uhakika – barabara hii hapa, shule hii hapa, darasa hili hapa – ili wananchi wenyewe wathibitishe kile kilichofanyika chini ya Rais Samia, Chama Cha Mapinduzi, wabunge, na madiwani,” alifafanua.
Aidha, Mhe. Kyombo alieleza kuwa tayari wana orodha ya miradi yote iliyotekelezwa katika kila kata pamoja na kiasi cha fedha kilichotumika, jambo ambalo litawasaidia wananchi kufuatilia maendeleo kwa uwazi na kutoa mrejesho kwa viongozi wao.
Vilevile, alitumia nafasi hiyo kuwashukuru madiwani wote kwa ushirikiano wao mzuri katika kusukuma mbele maendeleo ya Missenyi na kuwataka waendelee kudumisha mshikamano, huku wakijielekeza zaidi kwenye masuala ya msingi ya kuwahudumia wananchi.