Tarime, Juni 10, 2025.
Tabibu wa Kituo cha Afya Magena, Jacob Ibrahim Wankyo, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime akikabiliwa na tuhuma za kuomba na kupokea rushwa, kinyume cha sheria.
Kesi hiyo namba 13960/2025, ilisikilizwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Mheshimiwa Veronica Seleman, ambapo upande wa mashtaka ukiongozwa na Mwendesha Mashtaka kutoka TAKUKURU, Bw. William Lyamboko, uliwasilisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Jacob Wankyo anatuhumiwa kuomba hongo ya Shilingi 350,000 na kupokea Shilingi 200,000 kutoka kwa mgonjwa aliyekuwa anahitaji huduma ya upasuaji wa uzazi. Tuhuma hizo ni kinyume na Kifungu cha 15(1)(a) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 Toleo la 2022.
Bw. Lyamboko alieleza kuwa tabibu huyo alitumia nafasi yake vibaya kwa kutaka rushwa kabla ya kutoa huduma ya afya ambayo ni haki ya msingi ya mgonjwa.
Mshtakiwa alikana mashtaka hayo mahakamani na baadaye aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa, ikiwemo kuwa na wadhamini wawili waliotia saini bondi ya Shilingi milioni 4 kila mmoja.
Mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi Juni 26, 2025 kwa ajili ya kusikiliza hoja za awali.
TAKUKURU imeendelea kusisitiza kuwa haitasita kuwachukulia hatua wote wanaokiuka sheria kwa kutumia nafasi zao vibaya katika utoaji wa huduma kwa wananchi.