Pankaj Chauhan (wa pili kulia aliyevaa miwani), Meneja Mkuu wa Nas Tyre Services, akitoa zawadi ya vifaa vya betri za Amaron Solar kwa mmoja wa wageni waliohudhuria hafla ya uzinduzi rasmi wa betri hizo nchini Tanzania. Betri hizi zimekusudiwa kusaidia matumizi bora ya nishati safi ya jua.
Dar es Salaam, 10 Juni 2025
TANZANIA inaendelea kusonga mbele katika safari yake ya nishati safi huku suluhisho mpya zikichipuka sio tu kwa namna ya kukusanya mwanga wa jua, bali pia jinsi ya kuhifadhi na kutumia nishati hiyo katika sekta mbalimbali na maeneo ya mbali.
Ingawa paneli za sola zimekuwa zikionekana katika majengo mijini na vituo vya afya vijijini, mafanikio ya nishati safi nchini yanategemea sana teknolojia muhimu ya betri za hifadhi ya nishati.
“Sasa hivi nishati ya jua si ndoto ya baadaye tena – tayari imeanza kubadilisha maisha hapa Tanzania,” anasema Pankaj Chauhan, Meneja Mkuu wa Nas Tyre Services, ambao sasa wamekuwa wasambazaji rasmi wa betri za sola za Amaron. “Kinachosisimua zaidi kuhusu teknolojia ya betri ni namna tunavyopeleka umeme katika maeneo ambayo yalikuwa hayajafikiwa hapo awali kama vile migodini na mashambani – kuifanya sola isiwe tu rahisi kupatikana, bali iweze kubadilisha maisha ya watuna kuwaletea faida katika shughuli zao za kila siku.”
Serikali imekuwa ikionyesha dhamira yake kwa kuondoa ushuru kwenye bidhaa za sola – hatua muhimu katika kupunguza gharama na kuhimiza matumizi ya nishati safi. Pia, kuongezeka kwa mahitaji kutoka kwa kaya binafsi na biashara ndogo ndogo kumechangia kuimarisha nafasi ya sola kwenye mkakati wa kitaifa wa nishati.
Hata hivyo, changamoto kubwa inayobaki ni jinsi ya kuhifadhi nishati inayozalishwa wakati wa mchana ili iweze kutumika usiku au wakati wa mahitaji makubwa. Hapa ndipo teknolojia ya betri inavyopata umuhimu – kuwa kiungo kati ya jua na uhuru wa kupata umeme kwa saa 24.
“Betri inabadilisha sola kutoka kuwa kitu cha kutumia tu mchana hadi kuwa tegemeo la kudumu,” anaeleza Chauhan. “Hiyo ndiyo nguvu ya kweli ya sola – iwe ni kwa shule, hospitali, biashara ndogo, au hata minara ya simu na taa za barabarani.”
Wiki hii, Nas Tyre Services imetangaza uzinduzi rasmi wa betri za sola za Amaron hapa nchini. Betri hizi zinatengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu kutoka Amaron – kampuni yenye uzoefu wa kimataifa katika suluhisho za hifadhi ya nishati.
Betri za Amaron zinajulikana kwa uwezo mkubwa wa kutunza nishati, maisha marefu na kuto-hitaji matengenezo, hali inayozifanya kuwa suluhisho bora la hifadhi ya nishati kwa watumiaji wa sola nchini.
Chauhan anasisitiza kwamba uamuzi wa kuleta betri za Amaron unalenga kusaidia malengo ya taifa ya upatikanaji wa nishati safi kwa gharama nafuu na huduma za kiufundi zinazopatikana hapa nchini.
“Hili ni jambo kubwa kwa jamii ya Watanzania kwani pale ambapo teknolojia, mazingira na upatikanaji wa nishati vinakutana na kuinua maisha ya jamii hii ina maana kubwa katika maendeleo ya sekta ya nishati na kukua kwa uchumi.” Kadri Tanzania inavyozidi kuwekeza katika nishati safi, betri hizi zinaweza kuwa mkombozi wa taifa katika kuelekea kwenye nishati safi.