Dodoma
Maktaba Kuu ya Taifa ya Tanzania imeeleza kuwa machapisho yenye taarifa za madini yaliyopo hapa nchini ni hazina ya taifa na yanapaswa kusajiliwa ili kulinda uhalali wa taarifa hizo kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo na historia ya taifa kwa ujumla.
Hayo yameelezwa leo Juni 12, 2025 na Afisa Mwandamizi kutoka Maktaba Kuu ya Taifa Laura Ndomba wakati wa ziara ya Maafisa Waandamizi kutoka Makao Makuu ya Maktaba Kuu ya Taifa Ofisi za Dar es Salaam na Dodoma walipotembelea Ofisi za Wizara ya Madini Mtumba, jijini Dodoma.
Laura ameeleza kuvutiwa na wingi wa machapisho mbalimbali ya kitaalamu yanayotolewa na Wizara ya Madini pamoja na taasisi zilizo chini yake na kubainisha kuwa machapisho hayo yanatoa maarifa muhimu kuhusu sekta ya madini, ikiwa ni pamoja na tafiti, sera, miongozo, takwimu na taarifa za miradi ya kimkakati.
“Tunaona taarifa hizi kama hazina ya taifa. Ni muhimu zisajiliwe rasmi kupitia Maktaba ya Taifa ili kupata ulinzi wa kisheria, lakini pia kuziwezesha kupatikana kwa kizazi cha sasa na kijacho,” amesisitiza Laura.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Maktaba ya Taifa, usajili wa machapisho ya serikali si tu unahakikisha uhifadhi wa kumbukumbu, bali pia unalinda ubunifu wa kitaifa dhidi ya matumizi yasiyoidhinishwa. Aidha, ulipaji wa nakala kwa Maktaba ya Taifa husaidia kuimarisha hifadhi ya maarifa kitaifa kwa mujibu wa sheria ya maktaba.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Madini Asteria Muhozya amekiri kuwa kumekuwa na changamoto ya kutosajili machapisho kupitia Maktaba ya Taifa jambo ambalo lingesaidia kuongeza ufanisi zaidi katika usambazaji na uhifadhi wa baadhi ya machapisho, hasa yale ya kiufundi na tafiti.
“Kusajili machapisho yetu kupitia Maktaba ya Taifa itasaidia kuhakikisha taarifa zote muhimu zinapata ulinzi wa kisheria na zinapatikana kwa wananchi kwa urahisi zaidi kupitia majukwaa ya Wizara pamoja na Maktaba ya Taifa” ameongeza Asteria.
Ziara hiyo imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Wizara ya Madini na Maktaba ya Taifa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha taarifa za kimkakati zinahifadhiwa na kusambazwa kwa ufanisi kwa manufaa ya taifa zima.