Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameungana na Mawaziri wa Mambo ya Nje na Waratibu wa utekelezaji wa Mpango Kazi wa Jukwaa la Ushirikiano baina ya China na Afrika (FOCAC) kushiriki hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya Nne ya Kimataifa ya Biashara kati ya China na Afrika (CAETE) yanayofanyika kuanzia tarehe 12 hadi 15 jijini Changsha, China.
Kauli mbiu ya maonesho hayo yaliyofanyika sambamba na Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje na Waratibu wa Utekelezaji wa Mpango kazi wa FOCAC ni, _China na Afrika: Pamoja katika Mageuzi ya Kisasa (China and Afrika: Together towards Modernization).
Kampuni takribani kumi kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinashiriki maonesho hayo ya CAETE ambayo pamoja na masuala mengine yanatoa fursa ya kushiriki kwenye mikutano na makongamano ya maeneo makhususi ya bidhaa na huduma kama vile sekta ya miundombinu, madini, viwanda, ujasiriamali, kilimo, na nishati.
Akihutubia katika ufunguzi wa maonesho hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Wang Yi ameeleza kuwa CAETE itaongeza fursa nyingi katika ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na Afrika na kwamba siku zote China itaendelea kuwa imara kushiriki katika mabadiliko ya kimaendeleo Afrika na kuwa rafiki wa kweli katika kuifikia safari hiyo ya mafanikio.
Pia amesisitiza kuwa China katika ushirikiano wake na Afrika inaendeleza jitihada za kuufungua uchumi wa mataifa hayo kwa kuingia makubaliano ya kupunguza tozo za bidhaa na za afrika ili ziweze kuingia kwa wingi katika soko la China. Vilevile, China inaimarisha ushirikiano wake na Afrika kwa vitendo katika kukuza viwanda na mageuzi ya teknolojia.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa mawaziri hao kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho yaliyokuwa yakionesha bidhaa na huduma ambapo walishuhudia wafanyabishara takribani 4,700 kutoka China na kampuni 30,000 kutoka Afrika zikiendelea kujitangaza pamoja na kuuza bidhaa na huduma zao.