Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimemtunuku Shahada ya heshima Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayemaliza muda wake, Dkt. Akinwumi Adesina.
Dkt. Adesina ametunukiwa Shahada ya Falsafa ya Sayansi na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na Rais wa awamu ya Nne wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika mahafali ya 55, duru ya kwanza ya Chuo hicho, yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar Es Salaam.
Akisoma wasifu wa Dkt.Adesina kabla ya kutunukiwa Shahada hiyo Prof. Rwekaza Mukandala ameleza kuwa Dkt. Adesina ni mfano halisi wa muunganiko nadra wa taaluma bora, uongozi wenye maono na athari chanya katika maisha, sifa ambazo zinamfanya kutunukiwa shahada hiyo ya heshima.
Chuo hicho kimejiwekea utaratibu wa kutunuku shahada za heshima kwa watu wenye sifa na kukidhi vigezo kila baada ya miaka mitatu, kilimtunuku shahada hiyo Dkt. Adesina baada ya kutoa mchango mkubwa barani Afrika na duniani kwa ujumla katika eneo la Kilimo na fedha.
Prof. Mukandala alisema Dkt. Adesina mwenye shahada ya uzamivu ya Uchumi wa Kilimo ametoa mchango mkubwa katika mageuzi kwenye sekta za kilimo, Uchumi na fedha barani Afrika na kutolea mfano kuwa alipokuwa Waziri wa Kilimo nchini Nigeria mwaka 2011 alibuni mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanzisha mpango wa kuwapelekea wakulima ruzuku ya mbolea kwa njia ya kieletronoki kupitia simu za mkononi (e-wallet).
Alisema Mpango huo uliongeza tija katika sekta ya kilimo na kunufaisha zaidi ya wakulima milioni 11 kwa kuondoa ukiritimba na rushwa kwa watu wa kati wasio waadilifu.
Kuhusu mageuzi ya kiuchumi, Rais wa Benki ya AfDB baada ya kushika nafasi hiyo mwaka 2015 aliiwezesha benki hiyo kuongeza mtaji kutoka Dola za Marekani bilioni 93 mwaka 2015 hadi bilioni 208 mwaka 2019 ambapo chini ya uongozi wake alianzisha vipaumbele vitano vikijulikana kama 5’s yaani, Angaza na ipe nishati Afrika, lishe Afrika, kuza viwanda Afrika, Jumuisha Afrika na boresha maisha ya waafrika na kwamba vipaumbele hivyo vinasifika kwa kuleta athari chanya kwa watu zaidi ya milioni 565 barani Afrika.
Prof. Mukandala aliongeza kuwa wakati wa uongozi wake AfDB imekuwa benki kinara ya kufadhili miradi ya miuondombinu ambapo zaidi ya Dola za Marekani bilioni 55 zimetumika katika sekta ya miundombinu barani Afrika.
Alisema kuwa Benki hiyo katika uongozi wake, iliwekeza katika miradi ya usalama wa chakula ambapo inaelezwa kuwa zaidi ya watu milioni 100 walinufaika na mradi huo. Zaidi ya hapo, Benki hiyo ilitoa Dola za Marekani bilioni 3 kwa ajili ya kuimarisha sekta ya afya barani Afrika na nyingine kama hizo kwa ajili ya kuimarisha sekta ya dawa.
Kuhusu mageuzi ya kifedha, Dkt. Adesina licha ya kuwa mchumi wa kilimo, lakini ametoa mchango mkubwa kubadaili mifumo ya kifedha barani Afrika ili iwe jumuishi na kuwanufaisha makundi ya watu wa aina zote wakiwemo vijana, wanawake na wanavijiji.
Akiwa Rais wa AfDB alisanifu upya mifumo ya fedha ya ugharamiaji maendeleo barani Afrika kama kuongeza mtaji wa benki hiyo, kuzindua hati fungani ya jamii na kuanzisha mifuko ya dharura ya kukabiliana na majanga. Hatua zinazotajwa kuimarisha miradi ya miundombinu, afya, kilimo na nishati barani Afrika.
Kwa upande wa Tanzania, chini ya uongozi wake, AfDB imekuwa na ushirikiano mzuri na Serikalis katika mkakati wa kuimarisha miundombinu ili kujenga uchumi shindani na kuboresha sekta binafsi kwa ajili ya kuzalisha ajira. Kwa upande wa miundombinu, AfDB inasaidia uendelezaji wa miradi ya usafiri wa ardhini, majini na angani kama vile mradi Barabara ya mzunguko jijini Dodoma, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato na ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, kipande cha kuunganisha Tanzania na Burundi.
Kuhusu kuimarisha sekta binafsi, AfDB imekuwa mdau muhimu wa Tanzania katika kuimarisha sekta ya kilimo ambayo imeiwezesha Tanzania kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 128. AfDB pia inashirikiana na Tanzania katika kuendeleza Mradi wa Jenga Kesho iliyo bora (BBT) ambao umewawezesha vijana zaidi ya 11,000 kujishughulisha na kilimo cha kisasa nchini.
Akizungumza baada ya kupokea Shahada hiyo ya heshima, Dkt. Adesina ambaye ametajwa yeye na benki yake kama wadau wakubwa wa Tanzania, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumwalika kuja Tanzania, nchi ambayo amesema anaipenda na kwamba yeye ni mwananchi wa Tanzania.
Aidha, amekishukuru Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kwa heshima waliyompatia na kuwasisitiza wanafunzi takribani 842 waliotunukiwa shahada pamoja naye, kutumia maarifa waliyoyapata, kubuni mikakati ya kulipeleka mbele Bara la Afrika.