Geita
Wananchi wilayani Bukombe mkoani Geita wameeleza kunufaika na mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika mji wa Ushirombo mradi unaotekelezwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Bukombe, Mhe. Yusuph Mohamed ambapo amesema kuwa licha ya mradi huo kuupendezesha mji pia utasaidia wananchi kuyafikia maeneo na huduma mbalimbali kwa urahisi.
“Mji wetu unapendeza na tunaendelea kupokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami, napenda kumpongeza Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan pamoja na mbunge wa Bukombe ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu Mhe. Dotto Biteko kwa kuendelea kuleta fedha za kutekeleza miradi mbalimbali katika Wilaya hii”.
Naye, mkazi wa Bukombe, Dkt. Mohamed Kaji ameeleza kuwa barabara za lami katika mji huo zina umuhimu kwani zinawezesha wananchi kuzifikia taasisi mbalimbali kwa urahisi .
Akielezea manufaa ya mradi huo, Bi. Elizabeth Mwenda mkazi wa Bukombe ameipongeza serikali kupitia TARURA kwa kuendelea kuboresha mandhari ya mji huo unaozidi kupendeza siku hadi siku.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA wilaya ya Bukombe, Mhandisi Msoka Msumba ameeleza kuwa kwasasa wanaendelea na mradi huo wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika mji wa Ushirombo zenye urefu wa km 3.25 na kwamba kukamilika kwa mradi huo kutapunguza adha kwa wananchi hasa kipindi cha masika.
“Wilaya ya Bukombe inatekeleza miradi mbalimbali ukiwemo ujenzi wa barabara hizi, tunaendelea kuishukuru serikali kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi hii”, amesema Mhandisi Msoka.