Na. Stanley Brayton, WMUV
PWANI
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amewataka wafugaji kuachana na Ufugaji wa kizamani na kufuga kisasa ili kuongeza tija katika sekta ya mifugo nchini itakayoendana na mahitaji ya Soko ya sasa.
Akizungumza katika Ufunguzi wa Maonesho ya Kimataifa ya Ufugaji Kibiashara na Mnada wa Mifugo yanayoshirikisha nchi tatu za Tanzania, Kenya na Namibia, yaliyofanyika katika Ranchi ya Mbogo iliyopo Chalinze Mkoa wa Pwani, Mhe. Mnyeti, amesema Serikali awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sasa inaendelea kuhamasisha wafugaji kuachana na Ufugaji wa kizamani na kuingia kwenye Ufugaji wa kisasa wenye tija.
“Ni matumaini yangu kuwa wafugaji mtachangamkia fursa hii kwa kutafuta na kununua mbegu bora za mifugo zitakazowaletea tija zaidi kwenye ufugaji wenu kuliko kuendelea na Ufugaji wa kizamani usio na tija.” ameseama Mhe. Mnyeti
Aidha, Mhe. Mnyeti amesema maonesho hayo ya mifugo yamelenga kuhamasisha matumizi ya mbegu bora za mifugo ili kumwezesha mfugaji kuzalisha mazao mengi ya mifugo na kupata faida zaidi ili kuifanya Sekta ya Mifugo iweze kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa na kuwawezesha pato la mtu mmoja mmoja.
Vilevile, Mhe. Mnyeti amesema swala la Malisho ya Mifugo imekuwa changamoto na wafugaji wengi wanatembea na rundo kubwa la mifugo kwa ajili ya kutafuta malisho, lakini Ufugaji wa kisasa utasaidia kuwa na Mifugo michache yenye tija ambayo italeta faida kubwa kutokana na uzito na ubora wa mifugo kuliko kuwa na Mifugo mingi yenye uzito mdogo ambayo haina faida yeyote wala tija.
Katika hatua nyingine Mhe. Mnyeti amewataka wafugaji kutafuta mbegu Bora za Malisho na kuzipanda kwa wingi kwa ajili ya Mifugo yao ili Mifugo iweze kupata chakula Cha kutosha kitakachowafanya kuwa Bora zaidi.
Mhe. Mnyeti amehitimisha hotuba yake kwa kukishukuru Chama cha Wafugaji Ng’ombe Kibiashara, Ranchi ya Mbogo pamoja na wadau wengine kwa kuandaa na kufanikisha maonesho hayo ambayo yameambatana na mnada wa mbegu bora za mifugo zenye tija zaidi kwenye uzalishaji wa Mifugo Bora mana wameungana na Serikali katika kuhamasisha Ufugaji wa kisasa.