
……….
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, ametoa maelekezo kwa wakuu wa idara na vitengo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kuandaa majibu ya hoja na mpango kazi wa utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Akizungumza katika Baraza Maalum la kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24, Kanali Ahmed amesisitiza uwajibikaji na kuchukua hatua stahiki dhidi ya watumishi watakaobainika kusababisha hasara au hoja kwa uzembe.
Ameitaka menejimenti ya Manispaa ya Songea kuhakikisha taarifa za mwisho wa mwaka zinaandaliwa kwa kuzingatia viwango vya kihasibu vya kimataifa katika sekta za umma, huku wakifuata sheria, kanuni, na taratibu za fedha na manunuzi ili kuepuka hoja zisizo za lazima na kudhibiti uwezekano wa hoja kujirudia kila mwaka.
Pamoja na hayo, ametoa maagizo ya kushughulikia hoja 14 za miaka ya nyuma pamoja na maagizo mawili ya LAAK ambayo hayajatekelezwa kikamilifu, akisisitiza kuwa hoja hizo lazima zikamilike na kuwasilishwa kabla ya Septemba 30, 2025.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mary Makondo, amepongeza usimamizi mzuri wa fedha za umma kwa mwaka wa fedha 2023/24, ambapo halmashauri zote za mkoa wa Ruvuma zimepata hati safi kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Amesema mafanikio hayo ni matokeo ya weledi, uadilifu, na uzalendo wa timu za wataalamu, wakiongozwa kwa umakini na madiwani, wakurugenzi wa halmashauri, pamoja na sekretarieti ya mkoa, jambo ambalo linaendelea kuimarisha uwajibikaji na ufanisi katika usimamizi wa rasilimali za umma.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Mheshimiwa Michael Mbano, ameonyesha dhamira thabiti ya kushughulikia hoja mbalimbali zinazoikabili Manispaa hiyo, licha ya changamoto zinazohitaji bajeti na muda wa utekelezaji.
Pamoja na juhudi hizo, amebainisha kuwa anajivunia mafanikio makubwa katika kuongeza mapato ya Manispaa, ambapo kiwango kimepanda kutoka Bilioni 2.5 hadi kufikia kati ya Bilioni 9-10 kwa mwaka.