Mbinga-Ruvuma.
Wakulima wa mahindi Mkoani Ruvuma, wameiomba Serikali kufungua soko la kuuza mahindi mapema ili waweze kunufaika na bei nzuri badala ya kuuza kwa wafanyabiashara walianza kupitia mashambani kutaka kununua kwa bei ndogo isiyolingana na gharama kubwa ya uzalishaji.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema,Serikali ndiyo mkombozi mkubwa wa wakulima kwa sababu ndiyo inayonanunua mahindi kwa bei nzuri kati ya Sh.500 hadi 700 ikilinganisha na wafanyabiashara binafsi wanaonunua mahindi Sh.300 hadi 400 kwa kilo moja.
John Nchimbi mkulima wa kijiji cha Matiri Wilayani Mbinga amesema,kama Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula(NFRA)itachelewa kufungua soko wakulima wengi wataathirika kwa kuuza mahindi kwa wafanyabiashara wa mitaani kwa bei ndogo.
“tunaiomba Serikali kupitia NFRA ifungue soko la mahindi haraka ili kutnusuru tusipate hasara kubwa, baadhi ya wafanyabiashara wameanza kupita mashambani kutushawishi tuwauzie mahindi”alisema Nchini.
Mkulima mwingine Athanas Komba amesema,soko la mahindi likifunguliwa haraka itakuwa faraja kubwa kwa sababu watapata fedha kwa ajili ya kununua mahitaji ya wanafunzi kabla shule hazijafunguliwa.
Erasto Mapunda mkulima kutoka kijiji cha Magagura amesema,kuchelewa kufunguliwa kwa soko la mahindi kuna hatarisha maisha na afya ya wakulima ambao wanategemea kilimo kupata fedha ili kuendesha maisha yao ya kila siku.
“hatuna wasiwasi na serikali yetu kuhusu bei ya mahindi hata na usimamizi wa zoezi la ununuzi kwenye kanda yetu ya Songea,lakini tunachoomba Serikali itufungulie soko mapema ili tupate fursa ya kuuza mahindi yetu kwani tuna uhitaji mkubwa ya fedha kwa ajili ya maandalizi ya watoto wetu wanaotakiwa kurudi shule mwezi ujao”alisema Mapunda.
Agatha Mapunda,ameishauri Serikali kufungua mipaka ili wakulima wenye uwezo wapeleke mahindi kuuza nje ya nchi kwani uzoefu unaonyesha Serikali haiwezi kununua mahindi yote yanayozalishwa katika mkoa wa Ruvuma na meneo mengine hapa nchini.
Ameomba,kuwepo kwa mfumo utakowezesha soko la mahindi kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula(NFRA)kuwafikia na kuwanufaisha wakulima wadogo badala ya kuwanufaisha zaidi wafanyabiashara,madalali na wakulima wakubwa.
Sebastian Komba mkazi wa Lukarasi, ameishauri NFRA kuzingatia hali ya uzalishaji na jiografia ya Wilaya ya Mbinga kwani kituo pekee kinachotumika kununua mahindi ni Kigonsera ambacho hakimsaidii mkulima mdogo.
Amesema Halmashauri ya Wilaya Mbinga ina kata nane zenye uzalishaji mkubwa wa zao la mahndi ambazo ni Mkako,Kigonsera,Amanimakolo,Namswea,Muungano,Matiri,Lukarasi na Ruanda lakini kata ya Kigonsera tu ndiyo kuna kituo cha ununuzi wa mahindi chini ya NFRA.
Amesema,baadhi ya wakulima wanashindwa kufikia soko hilo kutokana na umbali na gharama kubwa za usafirishaji kutoka kwenye maeneo ya uzalishaji hadi kwenye kituo cha ununuzi hivyo kuwalazimu kuuza mahindi na mazao mengine wanayozalisha kwa bei ya chini.
Kanda ya Songea,inategemewa sana kwa uzalishaji wa mahindi kwani kilimo ndiyo uti wa mgongo na uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma.
Kwa mwaka wa fedha 2024/2025 NFRA kanda ya Songea ilipangiwa kununua tani 72,000 za mahindi,lakini hadi kufikia mwezi Desemba 2024, NFRA ilinunua tani 118,292 sawa na asilimia 164.3 ya lengo na kufanya akiba ya mahindi kufikia tani 196,498,737.
Katika msimu wa kilimo 2024/2025 bei za ununuzi wa mahindi zilianza kwa Sh.500 kwa kilo moja,lakini Serikali iliongeza bei hadi kufikia Sh.700 jambo lililowahamasisha na kuwavutia wakulima wengi kupeleka mahindi kwenye vituo vilivyopo chini ya NRFA.