Na Mwandishi Wetu
KAKONKO, Juni 19, 2025 — Mahakama ya Wilaya ya Kakonko imewahukumu watumishi wawili wa kituo cha afya Mtendeli kwa makosa ya rushwa na uhujumu uchumi, katika kesi ya Uhujumu Uchumi Na. ECO 9652/2025.
Washtakiwa hao ni Onesmo Janks Nimbuga (34), Muuguzi Mkunga, na Annie Newton Mabago (37), aliyekuwa Mganga Mfawidhi wa kituo hicho. Mahakama imewatia hatiani kwa makosa 22 ya kutumia nyaraka kwa nia ya kumdanganya mwajiri, pamoja na ubadhirifu na ufujaji wa mali ya umma, kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329.
Aidha, walikabiliwa pia na kosa la kughushi kinyume na vifungu vya 333, 335(a) na 337 vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Marejeo ya mwaka 2022.
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani, washtakiwa walihusika katika kuandaa malipo hewa kwa kughushi nyaraka zinazoonesha kuwa wamenunua betri ya sola aina ya N200 yenye thamani ya TSh 586,200/=, ilhali fedha hizo zilitumika kwa matumizi yao binafsi.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mh. Ambilike Japhet Kyamba alitoa hukumu hiyo na kuwaamuru washtakiwa kulipa faini ya TSh 1,000,000/= kila mmoja.
Kesi hiyo iliendeshwa na Bw. Jackson George Lyimo, Mwendesha Mashtaka wa Serikali kutoka TAKUKURU mkoa wa Kigoma.
TAKUKURU imesisitiza kuwa taasisi hiyo itaendelea kusimamia uwajibikaji na kuwachukulia hatua kali wote wanaotumia ofisi zao kujinufaisha kinyume cha sheria.