:::::::::
Na Mwandishi Wetu
Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa jukwaa la kwanza la siku mbili litakalojadili kwa kina matumizi ya akili bandia (AI) na mchango wake katika maendeleo ya taifa, likitarajiwa kufanyika Julai 28 na 29, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA Tanzania, Dk. Nkundwe Mwasaga, amesema jukwaa hilo linatarajiwa kuwashirikisha zaidi ya washiriki 500 wakiwemo wabunifu, wanafunzi, wadau wa sekta binafsi, viongozi wa serikali pamoja na wakulima.
Dk. Mwasaga amesema tukio hilo ni la kihistoria kutokana na kasi ya maendeleo ya teknolojia ya akili bandia ambayo kwa mara ya kwanza katika historia, inazalisha mifumo inayoweza kufikiri na kufanya maamuzi kwa namna inayofanana na binadamu.
“Tunataka kujadili kwa kina mustakabali wa matumizi ya akili bandia nchini, tukiwa na kaulimbiu isemayo ‘Twatengeneza kesho ya Tanzania: Akili bandia inayozingatia maadili na utawala kwa taarifa kwa maendeleo jumuishi ya taifa na jamii,’” alisema Dk. Mwasaga.
Katika kongamano hilo, mada mbalimbali zitajadiliwa ikiwemo matumizi ya kawaida ya akili bandia, kuchakata data, maadili katika AI, uwazi wa matumizi, changamoto za kampuni changa zinazojikita kwenye AI na namna ya kuzisaidia ili ziweze kuchangia uchumi wa kidijitali.
Aidha, alisema jukwaa hilo litatumika kujenga uwezo wa ndani katika kutumia na kuunda mifumo ya akili bandia, kuandaa sera salama za matumizi yake, kubadilishana uzoefu wa kitaalamu, na kutoa fursa kwa vijana na wabunifu kutumia teknolojia hiyo kujiajiri au kuajiriwa.
“Ni wakati sasa wa kuhakikisha tunajenga ujuzi kwa Watanzania kuhusu namna ya kutumia teknolojia hii kwa usalama, huku tukilinda taarifa binafsi za wananchi na kuimarisha mchango wa TEHAMA kwenye pato la taifa,” aliongeza.