*Mwanasheria Mkuu wa Serikali asisitiza utoaji wa elimu ya sheria kwa wananchi
RAIS Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amempongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mlezi wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania kwa kukilea chama hicho vizuri na namna anavyoitekeleza majukumu yake katika kutoa ushauri wa kisheria kwa Serikali.
Mhe.Dkt. Kikwete ameyasema hayo wakati wa Kongamano la Kitaifa la Sheria liliofanyika tarehe 21 Juni, 2025 katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo lililoratibiwa na Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA), limechagizwa na kauli mbiu ya Demokrasia kwa Vitendo:Sheria,Uwajibikaji na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Aidha, Mhe. Dkt Kikwete ameeleza kuwa kupitia kongamano hilo itakuwa ni fursa nzuri kwa wananchi kuweza kupata elimu ya masuala ya mbalimbali ya kisheria hususan Sheria za Uchaguzi na kuwewezesha wananchi na wadau kufahamu haki zao za msingi na kuongeza uelewa wa wananchi katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
“Kongamano hili ni fursa nzuri ya kuwawezesha wananchi kufahamu haki zao za Msingi na uelewa mpana kuhusu Sheria za Uchaguzi”. Amesema Mhe. Rais Mstaafu .
Katika hatua nyingine Mhe Dkt. Kikwete amekipongeza Chama cha Mawakili wa Serikali kwa kuandaa kongamano hilo ambalo litaendesha mijadala mbalimbali na kuwa sehemu ya kubadilishana mawazo kuelekea Uchaguzi Mkuu hivyo ni vyema kila mmoja atumie fursa hiyo kupata mambo mazuri yenye tija na kufanya Tanzania kuendelea kuwa kisiwa Cha amani
“Chama hiki nimeambiwa kina wanachama takriban 4,000 hili si jeshi dogo, kama taratibu za kijeshi hili ni zaidi ya brigedi. Kwa hiyo ninafurahi licha ya uchanga wenu mmefanya mambo makubwa.” Amesema Mhe. Rais Mstaafu Dkt. Kikwete
Mlezi wa Chama cha Mawakili wa Serikali na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe Hamza S. Johari ametaka Mawakili wa Serikali kutumia kongamano hilo katika kujenga na kukuza uelewa wa Wananchi na Watanzania kwa ujumla kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria yanayohusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
“Tulitumie kongamano hili katika kuwaelemisha Wananchi kuhusu na masuala mbalimbali ya kisheria hususani maboresho yaliyofanyika katika sheria Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024” amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewakumbusha Mawakili wa Serikali kuwa wao ni watu muhimu katika ustawi wa Jamii na Taifa kwa ujumla, huku akisisitiza kuwa wako kwenye chama kikubwa.
“Sisi Mawakili wa Serikali ni askari wa kalamu ndani ya chama kikubwa na kongamano hili limekuja katika kipindi muafaka kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini (Mb) ambaye alimwakilisha Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.Damas Ndumbaro amesema, kongamano hilo jumuishi litazungumzia kwa kina masuala ya Uchaguzi ujao litawawezesha wananchi kuongeza uelewa kuhusu sheria za Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.
Vilevile, Mhe, Sagini amekipongeza Chama cha Mawakili wa Serikali kwa kuja na ubunifu huo, pia amewahimiza wadau wengine wa Sheria ikiwemo Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusiana na masuala mbalimbali ya kisheria.
Awali, Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania, Wakili Bavoo Junus akiwasilisha salamu za chama hicho amesema kuwa lengo la hilo ni kujadili masuala ya kisheria na kutoa elimu kwa Watanzania ili wapate uelewa mpana kuhusu masuala ya Uchaguzi Mkuu.
Wakili Junus amesema, moja kati ya malengo ya kuanzishwa kwa Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA) ni kuwaunganisha Mawakili wa Serikali wanaotoka katika maeneo mbalimbali nchini na kuwezesha Mawakili hao kujadili namna bora ya kutoa huduma za kisheria kwa wananchi.
“Kwa sababu Serikali inawajibika kwa wananchi, kwa maana hiyo sisi ni mawakili wa wananchi.” Amesema Bw. Junus.