Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Watemi wa kabila la Wasukuma mara baada ya kutembelea Kituo cha Utamaduni na Makumbusho ya Wasukuma Bujora, Kisesa Mkoani Mwanza tarehe 21 Juni, 2025.
……………..
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kushiriki kikamilifu kulinda maadili kwa ajili ya ustawi wa jamii kwa kuwa jukumu hilo ni la Watanzania.
Taarifa iliyotolewa na Shaaban Kissu Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu imesema Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo wakati wa ufunguzi rasmi wa Tamasha la Utamaduni la Bulabo lililofanyika katika viwanja vya Bujora-Kisesa, Wilayani Magu.
Aidha, Rais Dkt. Samia amesema Serikali inatambua na kuthamini juhudi kubwa
zinazofanywa na wadau wa utamaduni pamoja na viongozi wa kimila katika kuhakikisha
utamaduni wa Tanzania unaenziwa na kurithishwa kizazi hadi kizazi.
Vilevile, Rais Dkt. Samia ameeleza Serikali inatambua umuhimu wa matamasha ya
utamaduni na itaendelea kuyatumia katika kudumisha na kuendeleza utamaduni, mila na
desturi za Watanzania.
Rais Dkt. Samia ameongeza kuwa utamaduni ndio msingi mkuu wa utambulisho na
mshikamano wa Taifa hususan katika kipindi hiki cha mabadiliko ya dunia katika nyanja
za kiteknolojia, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
Halikadhalika, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa Serikali inaendelea na juhudi za
kuhakikisha Tamasha la Bulabo linatangazwa na kutambulika kimataifa kutokana na
upekee wake katika kuhifadhi utamaduni.
Aidha, Rais Dkt. Samia amewapongeza waandaaji wa Tamasha la Utamaduni la Bulabo la
mwaka huu kwa maandalizi mazuri yaliyovutia wageni kutoka mataifa mbalimbali
yakiwemo Oman na Jamhuri ya Afrika Kusini, na hivyo kulifanya tamasha hili kuanza kusikika kimataifa.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amepongeza jitihada za Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuendesha mafunzo sambamba na Tamasha hilo
kuhusu umuhimu wa kulinda na kudumisha maadili, mila na desturi za Kitanzania, na
kueleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kurithisha utambulisho na tamaduni za Taifa
kwa vizazi vijavyo.
Mapema kabla ya kufungua Tamasha, Rais Dkt. Samia alitembelea Kituo cha Utamaduni
cha Bujora na Makumbusho ya Kabila la Wasukuma na kuzungumza na Machifu na
Watemi wa kabila hilo.
Rais Dkt. Samia amewaomba viongozi wa kimila, Machifu na Watemi kuendelea kuliombea
Taifa liendelee kuwa na amani, umoja na mshikamano wa Taifa.
Rais Dkt. Samia amehitimisha rasmi ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza na kuwashukuru
wananchi wote wa Mkoa huo kwa ushirikiano mkubwa na ukarimu waliomuonesha wakati
wote wa ziara yake ya kikazi Mkoani humo.