Nihifadhi Abdulla Zanzibar.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema usimamizi wa viwango vya bidhaa ni nyenzo muhimu ya kukuza bishara na kufikia masoko ya kimataifa.
Ameyasema hayo wakati akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kwenye hafla ya ufunguzi wa mkutano wa Baraza Kuu la 31 wa Shirika la Viwango Afrika (ARSO), uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip.
Amesema kufikiwa kwa viwango vya bidhaa ni jambo muhimu sana na ndio kichocheo cha watumiaji kuwa na uhakika wa usalama wa bidhaa wanazotumia sambamba na kuyafikia masoko makubwa sehemu mbalimbali ulimwenguni.
Amefahamisha kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha Taasisi ya Viwango Zanzibar ili itekeleze majukumu kwa ufanisi ikiwemo kusaidia ustawishaji wa biashara, kuongeza ushindani na upatikanaji wa masoko kwa bidhaa zinazozalisha hapa nchini.
Amesema jukumu kuu la usimamizi wa viwango ni kuchochea biashara barani Afrika, kukuza usalama wa watumiaji, kuimarisha ushindani wa biashara, kulinda mazingira, kuwezesha upatikanaji wa masoko na kuwasaidia wajasiriamali wadogo na wa kati kutekeleza kikamilifu shughuli zao.
Mhe. Hemed amefahamisha kuwa ili kufikia masoko ya nje wazalishaji wanapaswa kutimiza mahitaji ya soko hasa kuzingatia ubora, usalama, uaminifu, usafi wa mazingira na uthibitisho usiokuwa na mashaka.
Aidha, amesisitiza umuhimu utolewe katika kurahisisha mifumo ya udhibiti ya Afrika kuhusu viwango vya pamoja, uthibitishaji na kanuni za ubora chini ya taasisi kama vile Shirika la Viwango Tanzania(TBS), taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS), Umoja wa Viwango Afrika (ARSO) na miundombinu ya ubora wa bara la Afrika (PAQI).
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, ameipongeza ARSO kwa kuendelea kujitolea kuendeleza ubora wa kuunganisha miundombinu Afrika na kuwataka kufanya kazi kwa pamoja katika kuonesha mifumo ya udhibiti ya Afrika kwa ufanisi na kwa njia bora zinazochochea ubunifu na kusaidia ushindani wa Bara la Afrika.
Ametoa wito kwa kwa ARSO kupitia mkutano huo kuendelea kuweka nia ya pamoja ya kuunga mkono viwanda vidogo na vya daraja la kati kwa kuweka mazingira bora ya ukuwaji wao huku akisisitiza kuimarisha ushindani na uzalishaji wao kwa kuwa na mageuzi ya sera, mifumo ya kibiashara, kujenga uwezo na kuweka mifumo ya ubora ya udhibiti na kukuza utamaduni wa ubora wa viwango ambao ni muhimu katika soko.
Kwa upande wake waziri wa Biashara na Maendeleo ya viwanda Zanzibar Mhe. Omar Said Shaaban amesema kwa sasa viwango vya ubora sio suala la hiari ni suala la lazima hasa katika kuimarisha ubora wa bidhaa na huduma za Afrika na kuongeza uwezo wa ushindani Kimataifa pamoja na kulinda maslahi ya watumiaji.
Waziri Shaaban amesema Zanzibar ina mpango wa kuweka maabara yenye vifaa kisasa ili kuidhinisha viwango Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kwa kufundisha wataalamu wa viwango, sera, taratibu pamoja na Jumuiya ya Biashara katika kuongeza uwelewa kuhusu umuhimu wa viwango.
Amesema Kupitia mkutano wa ARSO, Zanzibar itaweka historia mpya ya ubora, ushindani na usalama ambapo kupitia utekelezaji Zanzibar itapiga hatua kubwa kuelekea mustakbali wa Afrika wa kuwa na biashara zenye viwango bora na kukidhi mahitaji ya soko la dunia.
Nae Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dkt. Ashura Kantunzi amesema kufanyika kwa mkutano huo kunatoa nafasi ya kutafakari kwa kina juu ya namna ya kuandaa mazingira ya biashara kwa kuzingatia mazungumzo, uwazi na heshima pamoja na kuhakikisha usawa zaidi kwa wazalishaji wa Kiafrika hasa biashara ndogo ndogo na za kati.
Dkt. Ashura amesema TBS na ZBS ina mpango wa kusaidia biasha ndogo na za kati kwa kutambua kuwa ndio injini ya uchumi waa nchi kwa kuwapa miongozo iliyorahisishwa ya viwango na mafunzo yaliyolenga kukidhi mahitaji ya ubora wa biashara chini ya AFCFTA na kuhakikisha faida ya biashara huria inawafikia wazalishaji wadogo ambao mara nyingi wanakabiliwa na chamgamoto mbali mbali za kibiashara.