Taasisi ya Ladies of New Millennium, ikiongozwa na Mwenyekiti Mama Tunu Pinda wame imeanza ziara ya kikazi mkoani Mwanza kwa ajili ya kutembelea miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) inayotekelezwa chini ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (PSSN).
Wakiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, wajumbe wa taasisi hiyo walitembelea Shule ya Sekondari ya Igogwe ambapo walishuhudia maboresho ya miundombinu ya elimu yanayowezeshwa na TASAF kupitia afua za kijamii.
Pia walikutana na vikundi vya wajasiriamali walionufaika na mpango huo, waliopata mafunzo ya ujasiriamali na mitaji midogo inayowawezesha kuendesha shughuli za kiuchumi na kuongeza vipato vyao.
Katika kuunga mkono juhudi za Serikali na TASAF katika kuinua hali za maisha ya walengwa, taasisi ya Ladies of New Millennium ilitoa mitungi ya gesi kwa baadhi ya walengwa wa mpango huo ikiwa ni sehemu ya mchango wao katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, ambao ni hatari kwa afya na mazingira.
Aidha, wajumbe hao walitembelea ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na kufanya mazungumzo na Katibu Tawala wa Mkoa Bw. Balandya Mayuganya, wakipata maelezo ya utekelezaji wa mpango huo na mchango wake katika maendeleo ya jamii mkoani humo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Shedrack Mziray, Mkurugenzi wa Mifumo, Tathmini na Mawasiliano wa TASAF, Bw. Japhet Boaz, alieleza kuwa mpango wa TASAF umeendelea kuwafikia wananchi wenye uhitaji mkubwa kwa kupitia afua mbalimbali zinazolenga kuongeza kipato, kuboresha huduma za kijamii na kujenga uwezo wa walengwa kushiriki katika maendeleo yao.
“Zaidi ya kaya milioni moja nchini zimenufaika na mpango huo kwa nyanja tofauti ikiwa ni pamoja na elimu, afya, lishe na ajira ya muda,” alisema.
Wajumbe wa Ladies of New Millennium walipongeza Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendeleza na kuimarisha jitihada za kupambana na umaskini kupitia TASAF. Vilevile waliisifu TASAF kwa usimamizi thabiti na utekelezaji madhubuti wa miradi inayogusa maisha ya wananchi wa kawaida.
Ziara hiyo imetoa fursa ya kuonesha mshikamano wa kijamii na kuhamasisha ushirikiano baina ya taasisi binafsi na Serikali katika kupambana na umaskini na kuendeleza maendeleo endelevu ya jamii.