Daktari Bingwa wa Tiba ya Magonjwa ya Dharura kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dkt. Evelyne G. Mapunda akionesha vifaa tiba vinavyotumika kumsaidia mgonjwa anayehitaji huduma dharura kupitia teknolojia ya kisasa, katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea kwenye viwanja vya Julius Nyerere, Dar es Salaam (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Mratibu wa Maabara ya Mafunzo ya Tiba ya Dharula MUHAS Gudy A. Hincha akionesha vifaa vinavyotumika kumsaidia mgonjwa anayehitaji huduma ya dharura.
Daktari wa Meno na Kinywa kutoka MUHAS Dkt. Denis Richard akimfanyia uchuguzi wa kinywa na meno mtoto aliyetembelea banda la MUHAS katika Maonesho ya Sabasaba.
………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, kimeendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala mbalimbali ya kiafya, ikiwemo namna ya kutoa huduma ya kwanza kwa wagonjwa wa dharura na matumizi ya vifaa tiba vya kisasa katika ufundishaji wa wanafunzi wa kada mbalimbali za afya.
Akizungumza na mwandishi wetu leo Julai 1, 2025 jijini Dar es Salaam katika Maonesho ya Sababasa yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere, Daktari Bingwa wa Tiba ya Magonjwa ya Dharura kutoka MUHAS Dkt. Evelyne G. Mapunda, amesema kuwa idara mbalimbali kutoka chuo hicho zinaendelea kutoa elimu ya afya kwa jamii na kueleza utekelezaji wa majukumu yao.
Dkt. Mapunda amesema kuwa wanatoa elimu kuhusu huduma za awali kwa wagonjwa wanaopata matatizo ya kiafya kama vile kisukari na degedege kabla ya kuwafikisha hospitalini ili kuokoa maisha yao.
“Kwa mfano, mtu anaweza kujeruhiwa na kutoka damu nyingi au kupata degedege, tunatoa elimu kuhusu huduma za dharura za awali ambazo mtu anaweza kumpa mgonjwa ili kumsaidia kuokoa maisha yake kabla hajapata huduma ya kitaalamu,” amesema Dkt. Mapunda.
Naye Daktari wa Meno na Kinywa kutoka MUHAS, Dkt. Fredrick Andrew, ameeleza kuwa wanatumia teknolojia ya kisasa katika kufundishia wanafunzi wa Shule Kuu ya Afya ya Kinywa, ikiwa ni pamoja na viti maalumu vya kutoa huduma za meno na vifaa tiba vingine vya kisasa.
Dkt. Andrew amesema kuwa katika maonesho hayo, wamejikita pia katika kufanya uchunguzi wa afya ya kinywa na meno, na kwa wale watakaobainika kuwa na matatizo makubwa watapewa ushauri na maelekezo ya kitaalamu.
“Tunashauri kuhusu matumizi sahihi ya dawa ya meno, aina ya mswaki, namna ya kusafisha meno, pamoja na aina ya vyakula vinavyoweza kuchangia matatizo ya meno kama vile vyakula vyenye sukari nyingi,” ameongeza Dkt. Andrew.
MUHAS imepiga kambi katika maonesho hayo ikiwa na vifaa tiba mbalimbali vya kisasa kwa lengo la kutoa elimu ya afya, kuonesha teknolojia mpya zinazotumika kufundishia wanafunzi pamoja na kutoa huduma kwa jamii.
Kwa upande wao, wananchi waliotembelea banda la MUHAS, akiwemo Bi Janeth John, wamesema wameridhishwa na huduma walizopokea, ikiwemo elimu ya namna ya kujikinga dhidi ya magonjwa ya kinywa na meno, pamoja na namna ya kutoa huduma za dharura kwa wagonjwa.