Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Tunduru Yusuf Mabena aliyekaa,akimuelekeza kada wa Chama hicho Dkt Juma Matindana namna ya kujaza taarifa kwenye fomu za kuomba kuchaguliwa kugombea Ubunge katika Jimbo la Tunduru Kaskazini.

Mfanyabiashara maarufu Boniface Chacha,akijaza fomu ya kuomba kugombea ubunge katika jimbo la Tunduru Kaskazini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi jana,kulia Katibu wa CCM Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Yusuf Mabena.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es slaa Dkt Juma Matindana kushoto,akipokea fomu kutoka kwa Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Tunduru Yusuf Mabena kwa ajili ya kuomba ridhaa ya Chama hicho kugombea Ubunge katika Jimbo la Tunduru Kaskazini Mkoani Ruvuma.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Yusuf Mabena kulia,akimkabidhi fomu mfanyabiashara maarufu Wilayani Tunduru Boniface Chacha Marwa kwa ajili ya kuomba kugombea Ubunge katika Jimbo la Tunduru Kaskazini.

Mwanachama wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Ziada Sadik Matwele kushotoa,akipokea fomu kutoka kwa Katibu wa Chama hicho Yusuf Mabena, kwa ajili ya kuomba kugombea Ubunge Jimbo la Tunduru Kusini katika Uchaguzi wa Mwezi Oktoba mwaka huu.
…….
Na Mwandishi Wetu,Tunduru
MHADHIRI Mwandamizi wa Chuo kikuu cha Dar-es slaam Dkt Juma Mohamed Matindana,ni miongoni mwa wanachama wa Chama hicho waliochukua fomu kwa ajili ya kuwania kugombea Ubunge katika Jimbo la Tunduru Kaskazini Mkoani Ruvuma kupitia Chama cha Mapinduzi.
Akizungumza jana kwenye ofisi za Chama cha Mapinduzi Matindana alisema,nia yake kubwa ni kuwa sauti ya wananchi wa Tunduru hasa wale wa kawaida ambao watashirikiana kutatua changamoto zilizopo katika jimbo la Tunduru Kaskazini.
Kwa mujibu wa Dkt Matindana ni kwamba, yeye ni Mwanachama wa chama cha Mapinduzi kuanzia mwaka 2003 na amekuwa kiongozi wa Chama hicho kama mjumbe wa Halmashauri kuu Wilaya na mlezi wa kata mbalimbali za kichama.
Alisema, kwa sasa ameona ni muda mfuaka yeye kurudi nyumbani kama mwakilishi wa Wananchi kwenye nafasi ya Mbunge kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Tunduru Kaskazini.
Amewaomba wanachama wa Chama hicho kumuunga mkono katika harakati za kugombea Ubunge wa Jimbo hilo na kuhaidi kuwa iwapo atateuliwa na kuchaguliwa atashirikiana na wananchi pamoja na Chama cha Mapinduzi kusukuma maendeleo.
Wakati huo huo Mfanyabiashara maarufu Wilayani Tunduru Boniface Chacha Marwa, ni miongoni mwa wanachama waliojitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea ubunge katika Jimbo la Tunduru Kaskazini.
Akizungumza na waandishi wa Habari Chacha alisema,amejitafakari na kujiridhisha kwamba ana uwezo wa kugombea Ubunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini na kwa kushirikiana na wananchi atahakikisha Jimbo hilo linapiga hatua kubwa kimaendeleo na kiuchumi.
Alisema,iwapo Chama cha Mapinduzi kitampa ridhaa na wananchi kumchagua kuwa Mbunge wao watalibadili Jimbo la Tunduru Kaskazini kuwa kitovu cha kiuchumi kutokana na uwepo wa rasilimali kubwa za madini na ardhi inayofaa kwa kilimo cha mazao ya kila aina.
Naye Kada wa Chama hicho Ziada Matewele ni miongoni mwa wanachama wa Chama hicho waliochukua fomu ya kugombea Ubunge katika Jimbo la Tunduru kusini.
Alisema, katika jimbo la Tunduru kusini kuna kero kubwa hususani wananchi kukosa soko la uhakika la kuuza mazao yao na kupitia yeye na Serikali watatua changamoto za wananchi wa Jimbo hilo.
Amekiomba Chama cha Mapinduzi kumpa kipaumbele wakati utakapofika kwa kuchagua yeye kama mgombea mwanamke kugombea Ubunge katika Jimbo hilo.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Tunduru Yusuf Mabena alisema,zoezi la kuchukua fomu linaendelea vizuri na jumla ya wanachama 15 wakiwemo wanawake 4 wamejitokeza kuchukua fomu.
Alisema,kwa upande wa Jimbo la Tunduru Kaskazini waliochukua fomu ni wananchama 6 na jimbo la Tunduru Kusini wamejitokeza wanachama 9.
Mabena alisema,kwa upande wa nafasi ya udiwani jumla ya wanachama 128 wamejitokeza kuchukua kwa ajili ya kuomba ridhaa ya Chama hicho kugombea udiwani kwenye kata mbalimbali.
Amewataka wanachama wenye sifa,kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu kwa ajili ya kuomba kuchaguliwa na Chama kwenye nafasi ya Udiwani na Ubunge.