Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kufanya tathmini ya kina ya utekelezaji wa miradi ya maji kwa kuzingatia changamoto halisi zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali.
Kunenge alitoa wito huo leo, Julai 2, 2025, wakati akifungua kikao kazi cha kupokea na kujadili mipango na mikakati ya DAWASA kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kilichofanyika katika ukumbi wa Destiny, Kibaha kwa Mathias, mkoani Pwani.
Amesisitiza kuwa tathmini yoyote ya miradi lazima itokane moja kwa moja na maoni ya wananchi pamoja na viongozi , badala ya kutegemea taarifa za ripoti peke yake ambazo mara nyingine hazioneshi uhalisia wa mambo.
“Tujitahidi kupata tathmini kutoka kwa wananchi na viongozi. Itakuwa ni jambo la kusikitisha kuwa na tathmini nzuri ilhali wananchi hawaridhishwi. Tathmini bora ni ile inayotoka kwa wananchi,” alisema Mhe. Kunenge.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuwa na uelewa wa kina kuhusu hali ya upatikanaji wa maji kwa wananchi, na pale changamoto zinapotokea, hatua zichukuliwe kwa haraka. Aidha, alihimiza umuhimu wa kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu miradi inayoendelea ili kuepusha malalamiko au upotoshaji wa taarifa.
Kunenge aliitaka DAWASA kupanga vipaumbele vyenye uhalisia na vinavyotekelezeka, ili matokeo ya tathmini yawe na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, alisema kuwa kikao hicho kililenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa miradi na kuweka mikakati ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mchango wake mkubwa kupitia Programu ya “Kumtua Mama Ndoo Kichwani” iliyowezesha kupatikana kwa zaidi ya Shilingi Bilioni 220 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maji.
Akizungumzia maendeleo ya miradi ya maji mkoani Pwani, Mhandisi Bwire alieleza kuwa Mradi wa Maji wa Mkuranga I umekamilika, huku Mkuranga II ukiendelea kutekelezwa. Aidha, Mradi wa Kisarawe wenye thamani ya Shilingi Bilioni 10.6 unaendelea kukamilishwa.
Pia alibainisha kuwa utekelezaji wa Mradi wa Maji kutoka Bwawa la Kidunda umefikia asilimia 31, sambamba na maandalizi ya Mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Rufiji, ambao unatarajiwa kuzalisha zaidi ya lita milioni 1.5 kwa siku – ukiwa suluhisho la muda mrefu kwa huduma ya maji katika Mkoa wa Pwani, hasa kutokana na ongezeko la viwanda na mahitaji ya maji.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon, alipokuwa akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, aliipongeza DAWASA kwa juhudi zake katika kutekeleza miradi ya maji. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kufanya tathmini kwa kila mtumishi mmoja mmoja, ili kutambua changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa miradi na kuzitatua mapema.
Kwa sasa, Mkoa wa Pwani umefikia mafanikio makubwa katika huduma ya maji safi, ambapo upatikanaji mijini umefikia asilimia 93% na vijijini asilimia 83% – mafanikio yanayotokana na juhudi za Serikali kupitia DAWASA katika kuboresha maisha ya wananchi.