Na Mwandishi Wetu
Wakulima kutoka wilaya za Newala na Ruangwa mkoani Mtwara wamehitimu mafunzo ya kuongeza thamani ya zao la korosho, yaliyoandaliwa na NMB Foundation kwa ushirikiano na Rabo Foundation pamoja na kampuni ya Prosperity Agro Industries Ltd.
Mafunzo hayo yalihitimishwa kwa hafla iliyohudhuriwa na viongozi wa serikali na taasisi mbalimbali, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Newala, Alhaji Rajabu Kundya ambaye alikuwa mgeni rasmi. Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Meneja Mkuu wa NMB Foundation, Nelson Karumuna, alisema lengo la programu hiyo ni kuwajengea wakulima uwezo wa kuongeza thamani ya mazao yao, hasa korosho, ili waweze kunufaika zaidi kiuchumi.
“NMB Foundation inaamini kuwa kuongeza thamani ya mazao ya wakulima ni hatua muhimu katika kuwawezesha kufikia soko lenye tija zaidi, kukuza kipato na kuimarisha maisha ya familia na jamii kwa ujumla,” alisema Karumuna.
Mkuu wa Wilaya ya Newala, Alhaji Rajabu Kundya, aliipongeza NMB Foundation na wadau wake kwa jitihada hizo, akisema kuwa mafunzo hayo ni chachu ya mapinduzi ya kilimo mkoani Mtwara. “Hiki ni kielelezo tosha cha ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali katika kuinua wakulima,” alisema Kundya.
Katika hafla hiyo, wakulima waliokamilisha mafunzo walikabidhiwa vyeti vya ushiriki kama ishara ya kuthibitisha uwezo wao mpya katika kuchakata na kuongeza thamani ya korosho. Miongoni mwao ni Asha Juta, Laurent Muya, Ismail Chibumbui, Rehema Saidi, na Asha Abrahmani waliopokea vyeti kutoka kwa Mkuu wa Wilaya pamoja na viongozi wengine waliokuwepo.
Kwa upande wake, Meneja Ubanguaji wa Bodi ya Korosho (CBT), Mangile Malegesi, alisisitiza umuhimu wa teknolojia na uongezaji thamani katika kukuza soko la korosho ndani na nje ya nchi. Naye Meneja Mkuu wa Prosperity Agro Industries, Haroun Maarifa, aliwahakikishia wakulima hao kuwa kampuni yake iko tayari kushirikiana nao katika hatua za uzalishaji na usindikaji.
Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za pamoja kati ya sekta binafsi na mashirika ya maendeleo kuhakikisha wakulima wa Tanzania hawabaki nyuma katika mnyororo wa thamani wa mazao yao.