…………
TAASISI ya Mtetezi wa Mama unatarajia kufanya Kongamano litakalowahusisha wanachama wake zaidi ya 3000 kutoka Tanzania Bara na Visiwani, lenye lengo la kuzungumzia masuala mbalimbali yaloyofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza kuhusu kongamano hilo Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Neema Karume alisema pamoja na mambo mengine kongamano hilo limelenga kupata taarifa za utekelezaji wa majukumu mbalimbali tangu kuanzishwa kwake.
Neema amesema kama ambavyo taasisi imejipambanua ikiwemo kuzungumzia masuala ya kimaendeleo yanayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo juhudi zake za kumtetea mwanamke na mtoto, taasisi hiyo inao wajibu wa kuja kwa jamii na kutoa mrejesho juu ya kile ambacho imekifanya.
“Kupitia kongamano hilo, wanachama wote mikoani kupitia viongozi wao watatoa mrejesho wa namna ambavyo wamehusika kumsaidia ‘Mama’ katika kile ambacho amekuwa akisisitiza ikiwemo kutete haki na usawa wa jamii ya wanawake na watoto” amesema Neema
Amesema Taasisi ya Mtetezi inaunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan za kuwaletea maendeleo watanzania akisisitiza kuwa tangu ashike kijiti cha madaraka miradi mingi ikiwemo ile ya kimkakati imezaa matunda kwa kuwanufahisha wananchi jambo ambalo wengi hawalidhania.
Amesema kupitia kongamano hilo, kauli ya Taasisi hiyo itakuwa kuwahamasisha wanachama wake ili wakirudi mikoani wakawahamasishe wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi Mkuu wa Oktoba na ‘KUTIKI’ kwa Rais Samia Suluhu Hassan
“Kama ambavyo tumekuwa tukisisitiza kuwa Oktoba tunatiki, hivyo ndivyo hata wanachama wetu tutasisitizana kwa pamoja ili tusifanye makosa, tuna kila sababu ya kumrejesha ‘Mama’ yetu ili aendelee yale mazuri ambayo tayari alikuwa anayafanya” amesisitiza Neema
Amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza na kuwaunga mkono kwa lengo moja la kufanikisha kongamano hilo linalotarajiwa kufanyika Dodoma Julai 26-27 Mwaka huu akiamini kuwa kupitia ushiriki wao wataweza kupata matokeo mazuri zaidi.
Aidha amesema kuwa hadi Sasa bado wanaendelea kufanya maandalizi ya kongamano hilo ikiwemo kuhamasisha michango baina ya wanachama wake kwa ajili ya kuliwezesha nauli huku pia aliwaomba wenye mapenzi mema na wenye nia ya kuwashika mkono kujitokeza.