Na Meleka Kulwa – Dodoma
HOSPITALI ya Benjamin Mkapa (BMH) imepata mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za afya, hususan huduma 17 za ubingwa bobezi, katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Mafanikio haya yameongeza upatikanaji wa huduma bora za tiba kwa wananchi wa Dodoma na mikoa jirani, na hivyo kuimarisha ustawi wa afya nchini.
Akiwasilisha taarifa ya mafanikio hayoleo Julai 10,2025 jijini Dodoma wakati wa kupokea ripoti ya Kambi ya Mabingwa Bobezi waliokwenda visiwani Comoro, Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hatua hiyo ni sehemu ya mafanikio ya diplomasia ya afya ya kimataifa, ambayo pia imeitangaza vyema Tanzania kimataifa kupitia utoaji wa huduma bora za tiba.
Mhe.Mhagama pia amezindua huduma mpya za Royal Clinics, zitakazotolewa kwa watu maarufu, wageni wa kimataifa, na kwa uchunguzi wa hali ya juu. ameeleza kuwa huduma hizo zitasaidia kuhamasisha Watanzania kutibiwa ndani ya nchi, na hivyo kukuza sekta ya Tiba Utalii.
“Hospitali ya Benjamin Mkapa imeendelea kuwa mfano wa utoaji huduma bora. Imetangazwa kuwa hospitali bora kitaifa kwa mwaka huu katika maadhimisho ya Wiki ya Afya,” amesema Mhe. Mhagama.
Aidha, Waziri amesifu ushirikiano kati ya Hospitali ya Benjamin Mkapa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), hususan kupitia mradi wa upandikizaji figo wenye thamani ya Shilingi bilioni 28, unaodhaminiwa na Shirika la Tokushukai kutoka Japan.
KAmesema kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa imesaini mikataba ya ushirikiano na taasisi za KCMC na JKCI, hatua inayolenga kuimarisha ubadilishanaji wa ujuzi wa kitabibu, utoaji wa huduma kwa mgonjwa, na matumizi ya tiba mtandao (telemedicine).
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi, amesema kuwa hospitali hiyo sasa inatoa huduma 17 za kibingwa na hupokea zaidi ya wagonjwa 1,200 kwa siku. Alibainisha pia kuwa hospitali hiyo imeanza kutoa figo kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine bila kufungua tumbo, pamoja na uwezo wa kupandikiza uloto kwa wagonjwa wa selimundu (sickle cell) bila hitaji la kufanana damu.
Prof. Makubi ameongeza kuwa hospitali inatarajia kujenga hosteli kwa wanafunzi wa ngazi ya diploma kwa kutumia mapato ya ndani, na kwa kushirikiana na UDOM itaandaa mkutano wa kitaifa wa upandikizaji figo na uloto mwaka huu.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Mpito wa Kamati ya Tiba Utalii Abdul Maliki Moleli, amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa kamati hiyo mwaka 2021, imefanikisha ukarabati wa miundombinu, kuongeza uelewa kwa wananchi, na kuimarisha ushirikiano kati ya hospitali za serikali na binafsi.
Ametoa rai kwa Serikali kuunda kamati ya kudumu, kuanzisha kitengo maalum cha uratibu, kupitisha sera rasmi ya Tiba Utalii, na kuandaa mwongozo wa utoaji Visa kwa wagonjwa wa kimataifa.