Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari amefanya ziara ya kutembelea maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Sabasaba Jijini Dar es Salaam, tarehe 10 Julai, 2025
Akizungumzia ushiriki wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu katika maonesho hayo Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa pamoja na masuala mengine Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inashiriki maonesho hayo kwa lengo kuu la kutoa elimu ya masuala ya Kisheria kwa Wananchi.
“Lengo letu la kuja kwenye maonesho haya ni kutimiza moja ya malengo yetu, ambayo ni kutoa elimu kwa umma ili waweze kufahamu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama mshauri mkuu wa Serikali na kazi ambazo Ofisi hii inafanya”. Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa sambamba na kutoa elimu kwa masuala ya kisheria kwa wananchi pia Ofisi hiyo inatoa huduma za utatuzi wa migogoro mbalimbali ya kisheria pamoja kushughulikia malalamiko mbalimbali ya wananchi.
“Kama yuko Mwananchi ambaye ana malalamiko hii ni fursa kwake aje kwenye banda letu tuna Mawakili mahiri wako hapa kwa ajili ya kutoa ushauri wa kisheria kwa wananchi.” Ameeleza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Vilevile, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wa mikataba mbalimbali ili kuhakikisha kuwa mikataba hiyo inafuata taratibu na sheria wakati wa utekelezaji wake na inakuwa na masilahi kwa wananchi.
“Sasa hivi tunachukua hatua za kuendelea kufuatilia mikataba mbalimbali ili kuhakikisha inatekelezwa ipasavyo na kuiepushia Serikali kuingia kwenye migogoro inayotokana na kutokuteleza mikataba ipasavyo”. Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Katika hatua nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametembelea Banda la Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria, Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuona shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Taasisi hizo katika maoenesho hayo.
Banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika maonesho ya Sabasaba liko katika Mtaa wa Media, Hema la Jakaya Kikwete banda namba 24, maonesho ya Sabasaba yalianza tarehe 28 Juni, 2025 yanaendelea hadi tarehe 13 Julai, 2025.