Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIBU wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) CPA,Amos Makalla,amesema mpaka sasa hakuna mtia nia yeyote aliyekatwa au kuenguliwa katika mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi ya ubunge,uwakilishi na udiwani hadi pale Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama hicho itakapokamilisha kazi yake.
Makalla ameyasema hayo leo Julai 13,2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuanza kwa vikao vya CCM ngazi ya Taifa.
Amesema mchakato bado uanendelea ndani ya chama na sasa Sekretarieti ya CCM inaendelea kupokea taarifa kutoka mikoa kisha kwenda Kamati kuu na baadae taarifa rasmi itawekwa wazi.
“Naomba nisisitize, kwa utaratibu wetu wa CCM mpaka sasa hakuna mtu ambaye ameenguliwa au kukatwa kama ambavyo inaripotiwa kwenye vyombo vya Habari, nimeona ( wameandika ) huyu kapenya au huyu kafyekwa, huyu hayupo kwenye tatu bora, kama nilivyosema mchakato huu wa uteuzi utahitimishwa na kikao cha Kamati Kuu ya CCM hapo ndio itakuwa mwisho wa kupata majibu ya mchakato mzima wa wagombea wanaoteuliwa kwenda katika kura za maoni” – amesema Makalla.
Aidha amewataka watia nia kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho mchakato bado unaendelea hadi pale Kamati Kuu itakapotoa uamuzi wa mwisho.
Amesema kuwa Kamati Kuu itakapohitimisha tutatoka kuwaambia walioteuliwa kwenda katika kura za maoni ndani ya CCM , zamani nyie mnajua ilikuwa watu wote wakigombea wote wanakwenda kupigiwa kura za maoni kwahiyo tumesema utaratibu wa sasa watateuliwa wachache ili kwenda kupigiwa kura za maoni
“Kama mnavyojua nafasi ni chache kulingana na idadi ya walioomba,hata ambao hawatateuliwa chama kinawathamini watia nia wote na wataendelea kuwa watulivu kwa chama chao”amesema Makalla
Katika hatua nyingine Makalla,ametolea ufafanuzi kuhusu Barua inayosambaa mtandaoni kujiuzulu kwa Balozi wa Cuba,Humphrey Polepole.
Makalla amesema kuwa ameiona barua ya Balozi wa Cuba,Humphrey Polepole mtandaoni na kwamba yeye mwenyewe ndio mwenye kuthibitisha uhalali wake.
Amesema kuwa endapo atathibitisha kama ni ya kwake maudhui ni ya kwake ni utashi wake lakini ambalo limemfurahisha ni kwamba amemalizia kwa kusema atabaki kuwa mwanachama muadilifu wa CCM.