Na. Mwandishi wetu – Algeria.
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeendelea kunadi vivutio na fursa za uwekezaji katika Maonesho ya Kimataifa ya “The 22nd INTERNATIONAl EXHIBITION OF TOURISM AND TRAVEL – SITEV 2025 yanayofanyika katika viwanja vya SAFEX
Exhibition Centre nchini Algeria.
Wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya bara la Afrika wameshiriki maonesho haya ambapo baadhi yao wametembelea banda la Ubalozi wa Tanzania na kupata taarifa muhimu kuhusu vivutio vya Utalii, fursa za uwekezaji na taratibu za kufika Tanzania kwa ajili ya Utalii.
Aidha, Mheshimiwa Iman Salum Njalikai Balozi wa Tanzania nchini Algeria aliwataka washiriki hao kuhudhulia maonesho ya aina hiyo ili kuvidana vivutio vya utalii vinavyopatikana Tanzania hususani vinavyopatikana katika Hifadhi za Taifa.
Mhe. Balozi aliongeza kuwa shirika la ndege nchini Algeria lina mpango wa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kuja Tanzania.
Vilevile, vyombo habari kadhaa vilivyokuwa katika maonesho hayo, viliweza kukusanya maudhui kutoka kwa wataalamu wetu juu ya shughuli za uhifadhi, utalii na fursa za uwekezaji na kuzirusha katika Runinga za Algeria na kwenye mitandao yao ya kijamii.
Katika maonesho hayo pia viongozi waandamizi wa Algeria akiwepo Waziri wa Utalii na Sanaa Bi. Horia Medahi, walifika katika banda la Ubalozi wa Tanzania nchini humo ili kupata taarifa mbalimbali za sekta ya utalii na mawanda yake.
Maonesho hayo yaliyoanza Julai 12, 2025 yanatarajia kuhitimishwa kesho Julai 15, 2025.