Na Fauzia Mussa
Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘B’, Amour Yussuf Mmanga, amewataka wananchi kudumisha amani na utulivu kuanzia sasa hadi kufikia Uchaguzi Mkuu ujao, akisisitiza kuwa ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha taifa linaendelea kubaki katika hali ya amani na usalama.
Akizungumza katika bonanza la mbio za ngalawa lililofanyika katika bahari ya Fumba, Shehia ya Fumba, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria, Mmanga alisema kipindi cha uchaguzi kimekuwa na historia ya kuibua vurugu na changamoto za kiusalama, ambapo vijana hutumiwa kwa kiasi kikubwa kuvuruga amani.
“Hakuna mbadala wa amani zaidi ya shari na vita. Vijana ndio hutumika zaidi kuvuruga amani katika mataifa mengi. Tunapaswa kuwa makini tusikubali kutumiwa kwa madhara ya nchi yetu,” alisema Mmanga.
Aliwaasa vijana kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani, hasa katika kipindi hiki kinachoelekea uchaguzi, akibainisha kuwa machafuko mara nyingi huathiri zaidi makundi maalum kama wanawake na watoto.
Mmanga aliipongeza Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria kwa kushirikiana na Legal Services Facility (LSF) kuandaa tukio hilo ambalo limeshirikisha makundi mbalimbali, Pamoja na mambo mengine likiwa pia na lengo la kueneza ujumbe wa amani na haki kwa jamii.
“Hili ni tukio muhimu linalowawezesha wananchi kuelewa haki zao na kutatua migogoro yao kwa njia ya amani. Nawashauri waliokumbwa na changamoto za kisheria watumie wasaidizi wa sheria waliopo katika maeneo yao kupata msaada,” aliongeza.
Aidha, Mmanga alitoa wito kwa wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na serikali za mitaa ili huduma za msaada wa kisheria ziwafikie wananchi kwa haraka zaidi.
Alisema atahakikisha anawakutanisha wadau hao na wananchi wake ili kila mmoja afurahie matunda ya uwepo wa wasaidizi wa sheria katika jamii.
Kwa Upande wake Hanifa Ramadhan Said, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, alieleza kuwa lengo la bonanza hilo ni kuwaunganisha wananchi wa Fumba na vijiji jirani na watoa huduma wa kisheria, ili wapate nafasi ya kueleza changamoto zao na kusaidiwa kwa njia ya kisheria.
“Wasaidizi wa sheria wako karibu na jamii na wanasaidia kutatua changamoto mbalimbali katika ngazi ya jamii, hata kwa wale wasioweza kumudu gharama za huduma za kisheria,” alisema Hanifa.
Naye Bakari Omar Hamad kutoka LSF alisema uwepo wa wasaidizi wa sheria ni nguzo muhimu ya maendeleo kwa kuwa unasaidia wananchi kudai haki zao kwa misingi ya amani na usawa.
Alisisitiza dhamira ya LSF kuendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha huduma hiyo inaendelea kupatikana kwa wote.
Kauli mbiu ya Wiki ya Msaada wa Kisheria mwaka huu ni: “Nafasi ya Wasaidizi wa Kisheria Katika Kukuza na Kulinda Amani ya Nchi Yetu”, na kilele chake kinatarajiwa kufanyika Julai 18, 2025.