Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amemtaka mkandarasi wa mradi wa maji wa miji 28 wilayani Mafinga kampuni ya Jandu Plambers LTD kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi ili kufanikisha hitaji la huduma ya majisafi kwa wakazi wa Mafinga kwa wakati.
Mradi huo katika mji wa Mafinga ni sehemu ya mradi mkubwa wa miji 28 nchini ikitarajia kuongeza asilimia tano ya huduma ya maji mijini kutoka asilimia 91.6 ya sasa na kwa upande wa vijijini mradi utaongeza asilimia 3 kufikia 86.
Aweso ametoa maelekezo hayo akikagua mradi huo ambao unatekekezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 48.
Amesema mradi huo wa maji una umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Mafinga kwani utakapokamilika utawezesha huduma ya majisafi katika mji wa Mafinga kufika asilimia 95 kutoka 65 zinazopatikana kwa sasa.
Ameongeza kuwa lengo la Serikali ya awamu ya sita ya Rais Dkt. Samia ni kuona jamii ya Watanzania inafaidika na matunda ya uwekezaji mkubwa unaofanywa katika sekta ya maji hivyo wakandarasi wanapaswa kutafsiri malengo hayo kwa kuongeza kasi ya utekekezaji.
Waziri Aweso katika ukaguzi huo ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri ambaye amesisitiza kuwa changamoto mbalimbali zilizokuwepo katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huo zimetatuliwa hivyo mkandarasi anapaswa kuonesha uwezo wake kwa kukamilisha mradi kwa wakati.