Na Baltazar Mashaka, Mwanza
Kongamano la kitaaluma kuhusu nafasi ya ubia katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050 linatarajiwa kufanyika kesho jijini Mwanza, likihusisha wadau kutoka sekta mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo (25.07.2025), Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Lupa Ramadhani, alisema kongamano hilo ni hatua ya awali katika utekelezaji wa dira hiyo, likilenga kupanua wigo wa ushiriki wa wananchi kwenye mijadala ya maendeleo na kuhimiza uwajibikaji wa pamoja katika ujenzi wa taifa.
“Wiki iliyopita, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050. Dira hiyo inatoa msisitizo mkubwa kwa dhana ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), kwa kuwa maendeleo ya kweli yanahitaji ushiriki wa kila Mtanzania, uwazi na utawala bora,” alisema Dkt. Ramadhani.
Aliongeza kuwa kongamano hilo ni la kimkakati na linalenga kuchambua nafasi ya PPP katika safari ya maendeleo ya taifa. Pia litajadili changamoto na fursa zilizopo kwenye mifumo ya sasa ya PPP, kujenga mwafaka kuhusu mikakati ya kuoanisha juhudi za ubia na vipaumbele vya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na ya umma.
“Kongamano hili litasaidia kukuza uelewa wa pamoja kuhusu umuhimu wa PPP katika kufanikisha malengo ya taifa. Tutashindanishwa hoja mbalimbali, tukijadili kwa kina na kuhamasisha lugha moja ya kitaifa kuelekea Dira ya 2050,” alieleza Dkt. Ramadhani.
Alisema mjadala huo utajikita kwenye maeneo makuu matatu: Dhana ya PPP na nafasi yake kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050,PPP katika kukuza uwekezaji na ufanisi wa uendeshaji wa serikali za mitaa na afasi ya sekta binafsi na mitaji ya nje katika ujenzi wa uchumi wa Tanzania
“Tuna matarajio ya kuwa na washiriki wapatao 300. Hili ni jukwaa wazi kwa wakazi wa Mwanza na Watanzania wote kushiriki kwa lengo la kuchochea mabadiliko chanya ya kimaendeleo,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Habari wa PPP, Chelu Matuzya, alisema kongamano hilo limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) na Kituo cha Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi.