KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amekubali kujiunga na timu ya Simba kwa mkataba wa miaka miwili, baada ya kukataa kusaini mkataba mpya na klabu yake ya sasa, kwa mujibu wa chanzo chetu.
Chanzo hicho kimesema kwamba, mchezaji huyo ambaye pia anaichezea timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ameshafikia makubaliano binafsi ya klabu ya Simba, ambapo kinachosubiriwa ni taratibu nyingine ili kukamilisha dili hilo.
“Sasa ni juu ya Simba kufikia makubaliano na Azam au Fei Toto atafute njia ya kuvunja mkataba wake kwa amani,” kilisema chanzo hicho.
Taarifa zinasema kuwa Fei Toto anataka kwenda kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na kikosi cha Simba chini ya kocha, Fadlu Davids.
Sakata la usajili wa mchezaji huyo limekuwa ni endelevu tangu msimu uliopita, ambapo klabu za Simba, Yanga na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini zikionekana kumhitaji.
Msimu huu pia klabu hizo hizo zilionekana kujaribu tena kutaka kumchukua, huku Azam nayo ikimwekea ofa mpya nono, kwani bado ana mkataba wa mwaka mmoja, lakini mwenyewe amekuwa akipiga chenga.
Hivi karibuni kulikuwa na taarifa za Fei Toto kuamua kubaki Azam ili amalizie mkataba wake ili aondoke msimu ujao akiwa huru na hii ni baada ya kuongea na kocha mpya, Florent Ibenge, kabla ya taarifa mpya za kukubali kutua Simba, huku kinachotakiwa sasa ni kuvunja mkataba uliobakia.
Wakati hayo yakiendelea, klabu ya Simba imesema kukaa misimu minne bila kombe au taji lolote inatosha, na sasa hataki hilo litokee tena msimu ujao, kwa maana hiyo inatengeneza kikosi bora na madhubuti ambacho kitakidhi matarajio ya wanachama na mashabiki wake.
Akizungumza jana, Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema kuwa wameshachoka kukaa misimu minne bila taji lolote, hivyo msimu wa 2025/26, wataingia kwa nguvu zote, akitambia usajili mkubwa unaofanywa na Kocha Mkuu, Fadlu kuelekea msimu ujao.
“Huu ni msimu wa nne tumemaliza bila kupata ubingwa wa Tanzania, au taji lolote la ndani, tuseme tu inatosha sasa. Miaka minne ya ukame inatosha, kuanzia msimu wa 2025/26, tumepanga uwe ni msimu wa mafanikio kwetu, hauwezi kuwa hivyo bila kuwa na wachezaji wazuri, bora, kutengeneza timu madhubuti, ndiyo maana hata maandalizi yetu yameanza mapema, mwishoni mwa mwezi Julai, huku ligi ikitarajiwa kuanza Septemba, maana tuna mwezi mzima na wiki mbili, ambazo tukizitumia vizuri, tunatengeneza kikosi imara kwa ajili ya michezo ya kimataifa na ya ndani,” alisema Ahmed.
Alisema siku yoyote kuanzia leo Jumatatu, wataanza kutangaza wachezaji waliosajiliwa.
“Tupo kwenye awamu ya pili ambayo ni ya kutambulisha wachezaji wapya, ambapo wakati wowote kuanzia Jumatatu (leo) tutaanza kuwatangaza. Tumefanya usajili mkubwa kwenye kikosi chetu msimu huu. Nikizungumzia usajili mkubwa siyo kuleta wachezaji wengi, hapana, ninamaanisha wachezaji bora,” alisema.
Hata hivyo, alisema Simba haijamaliza kuaga wachezaji ambao hawatowahitaji kuelekea msimu ujao, akifafanua kuwa safari hii kila kinachofanywa ni kwa matakwa ya kocha Fadlu na si vinginevyo.
“Kila mmoja anafahamu wachezaji ambao tumeachana nao, wameshaondoka, wamekwenda kutafuta malisho sehemu nyingine, lakini bado hatujamaliza kuwaondoa wale ambao tunakusudia kuwaacha, tunategemea kuanzia kesho (leo Jumatatu), tutakuwa tumemaliza kabisa wote ambao hatuna mpango nao kwa msimu ujao.
The post BHAASSIIIII….FEI TOTO MIWILI SIMBA SHWAAA….AZAM FC HAWAAMINI MACHO YAO😅😅…. appeared first on Soka La Bongo.