CHICAGO: MSHAMBULIAJI wa Mashetani wekundu Manchester United Rasmus Hojlund anasema angeweza kufanya vizuri zaidi angepata msaada katika safu ya ushambuliaji ya Manchester United misimu iliyopita akisisitiza yuko tayari zaidi kwa ushindani katika nafasi yake kuu ya ushambuliaji.
Baada ya saa 48 za tetesi kuhusu United kusaka ‘straika’ huku Mslovenia Benjamin Sesko akipewa nafasi ya kutua klabuni hapo baada ya mazungumzo kuanza baina ya United na RB Leipzig. Hojlund alijibu kwa vitendo ndani na nje ya uwanja.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Denmark alifunga bao moja na nusura apate la pili wakati Klabu yake ilipoichakaza Bournemouth 4-1 Uwanja wa Soldier Field jijini Chicago alfajiri ya leo katika mchezo wao wa pili wa mfululizo wa michezo ya Premier League Summer Series inayopigwa nchini Marekani.
“Mpango wangu uko wazi ni kukaa na kupigania nafasi yangu kwa vyovyote vile. Sina hofu na Ushindani ni sawa Huniimarisha. Nimejinoa na niko tayari zaidi. Msimu uliopita umepita lakini labda ningekuwa na msaada kidogo tu ningefanya vizuri” alisema Hojlund baada ya kutafuta kwa makusudi vyombo vya habari kwenye ushindi dhidi ya Bournemouth.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 alifunga mabao 10 katika mechi 52 za michuano yote msimu uliopita United ilipomaliza kampeni mbaya ya Ligi Kuu katika nafasi ya 15 lakini ameapa kusalia na kupigania nafasi yake katika kikosi cha Ruben Amorim. Tangu ajiunge na United mwaka 2023, Hojlund amefunga mabao 26 katika mechi 95 za mashindano.
The post Hojlund ajitetea kiwango kibovu United first appeared on SpotiLEO.