Kocha wa Azam Florent Ibenge.
KOCHA maarufu kwenye soka la Afrika, Florent Ibenge, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, juzi alianza rasmi kukinoa kikosi cha Azam FC kwa mara ya kwanza, huku akiahidi makubwa na kuomba ushirikiano kwa wachezaji wenyewe pamoja na benchi la ufundi.
Kocha huyo za zamani wa Timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, AS Vita ya nchini humo, RS Berkane ya Morocco na Al Hilal ya Sudan, alianza kukinoa kikosi hicho juzi kwenye Uwanja wa Azam Complex, akiwa na baadhi ya wachezaji, wengine wakiwa bado hawajafika na baadhi wakiwa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa, Taifa Stars.
“Leo yalikuwa ni mazoezi yetu ya kwanza, tumeanza kambi ya msimu mpya, nimepata fursa ya kuwaona wachezaji. Nimewaona baadhi ya wachezaji nawasubiri wengine ambao hawajafika, na ambao wako kwenye timu ya taifa, baada ya hapo tutakwenda Arusha kujifua kule.
“Kila kitu nilichokiona ni kizuri na mazingira ni mazuri pia, nadhani tukiwa na ushirikiano kati ya wachezaji wenyewe kwa wenyewe, pamoja na benchi la ufundi, tutafanya vizuri sana,” alisema kocha huyo.
Katika hatua nyingine, Ibenge ametangaza rasmi kumjumuisha Kocha wa timu ya Vijana ya Azam FC ya wachezaji wenye umri chini ya miaka 20, Kassim Liogope, kuwa sehemu ya benchi lake la ufundi kuelekea msimu mpya wa mashindano wa 2025/2026.
Liogope, ambaye ni mtaalam wa kukuza vipaji chipukizi, anajivunia mafanikio makubwa baada ya kuiongoza Azam U-20 kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vijana msimu uliopita, pia ni mzoefu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akiwa na timu ya Dodoma Jiji kabla ya kujiunga na Azam.
Hivyo Liogope anaungana na Ibenge ambaye msimu uliopita aliiongoza Al Hilal kufika robo fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika, kabla ya kutolewa na Al Ahly ya Misri, ambapo kwenye hatua za makundi ilikuwa pamoja na timu za Yanga, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na MC Alger ya Algeria.
Kocha huyo aliiongoza Al Hilal kumaliza kinara wa Kundi A, ikiwa na pointi 10. Ilitolewa kwa jumla ya mabao 2-0, ikichapwa bao 1-0 katika michezo miwili ya nyumbani na ugenini dhidi ya Al Ahly.
Ana kazi kubwa ya kuvunja mwiko wa klabu hiyo ambayo haijawahi kutinga hata hatua ya makundi ya mechi za kimataifa, iwe Ligi ya Mabingwa au Kombe la Shirikisho.
Meneja wa klabu hiyo, Rashid Nguya, alisema kabla ya mazoezi kulikuwa na kikao cha kutambulishana, kabla ya kocha huyo kutoa nasaha.
“Kabla ya mazoezi tulifanya mkutano wa kutambulishana kwa wachezaji pamoja na benchi lote la ufundi, wachezaji wamemfurahia sana mwalimu, wamempokea vizuri, yeye pia amekuwa na furaha sana. Amewaambia jinsi ya kuwa na ushirikiano ili kuweza kufikia malengo,” alisema meneja huyo.