NAIROBI: ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania,(Taifa Stars) ambaye kwa sasa anainoa Police FC ya Kenya, Etienne Ndayiragije amepongeza uamuzi wa Simba kumsajili kiungo wa klabu hiyo Mohammed Bajaber, akisema ni hatua sahihi kwa timu hiyo kubwa ya Tanzania.
Bajaber, ambaye alikipiga katika kikosi cha Police FC chini ya kocha Ndayiragije, inasemekana tayari amesaini mkataba kujiunga na Simba katika dirisha hili la usajili. huku Kocha huyo akisema Simba wamepata mchezaji mwenye uwezo mkubwa ambaye atakuwa msaada mkubwa kwa kikosi hicho.
Ndayiragije amefichua kuwa mazungumzo ya uhamisho wa Bajaber yalifanyika kwa uwazi na uungwana kati ya Simba na klabu yake, na kwamba baada ya kufikia makubaliano, mchezaji huyo aliruhusiwa kujiunga na miamba hiyo ya soka Tanzania.
“Simba walifanya mazungumzo ya biashara na klabu ya Police, tuliridhia kwa sababu ni fursa nzuri kwa mchezaji mwenyewe. Sasa naamini tayari ameshasaini na yupo tayari kwa changamoto mpya,” amesema kocha huyo.
Kocha Ndayiragije amesisitiza kuwa Bajaber ana sifa zote muhimu kwa mchezaji wa kiwango cha juu – ana akili ya uwanjani, uwezo wa kupiga pasi sahihi, na kujituma muda wote akiwa uwanjani, hivyo mashabiki wa Simba watarajie mambo makubwa kutoka kwake.
Kwa hatua hiyo, Simba inaonekana kuendelea kujijenga vyema kuelekea msimu ujao, ikiwa ni sehemu ya maboresho ya kikosi chini ya kocha wao Fadlu Davids, huku wakilenga kufanya vizuri katika mashindano ya ndani na kimataifa.
The post Kocha Taifa Stars: kwa Bajaber, Simba mmeula first appeared on SpotiLEO.