Yanga juzi ilimtambulisha kocha mpya, Romain Folz kuchukua nafasi ya Miloud Hamdi aliyeondoka katika timu hiyo mara baada ya msimu kumalizika.
Hamdi mmoja wa makocha bora aliyepita Yanga, aliondoka akiwa na heshima baada ya kutwaa makombe matatu katika muda mfupi.
Ujio wa Folz raia wa Ufaransa, ni ishara Yanga imerudi kule ilipokuwa wakati ilipomuajiri Kocha Saed Ramovic raia wa Ujerumani, ingawa hakudumu na timu hiyo na hakutwaa kombe lolote.
Folz anapewa nafasi kubwa ya kuipeleka Yanga katika nchi ya ahadi kutokana na mbinu zake, ujuzi na uzoefu alionao kwenye soka la kisasa, akiwa ameshakaa na makocha kadhaa wakubwa, lakini amewafundisha wachezaji wenye majina makubwa.
Pamoja na kwamba hana mafanikio makubwa sana katika soka akiwa kama kocha mkuu, lakini kitendo cha Yanga kumleta kocha huyo ni kwenda na soka la kisasa linavyotaka kwa sasa.
Dunia ya sasa ya soka haina tofauti kubwa sana na matumizi ya kompyuta, simu au vifaa vingine vya umeme ambavyo vimekuwa vikibadilika kila kukicha, hivyo ndiyo soka linavyobadilika dunia nzima na makocha wengi sasa ni wale ambao wamekubali kubadilika na teknolojia inavyotaka.
Lakini hauepuki kwa sasa kusema kuwa timu hiyo ya Jangwani, imehama na kuwafuata wapinzani wao Simba ambao walishtuka mwanzoni tu mwa msimu uliopita kutoka zama za kale na kuhamia kwenye zama za sasa la kukumbatia majkocha vijana. Folz ni kijana zaidi akiwa na miaka 35 tu.
Dunia ya sasa inahitaji makocha vijana wenye ujuzi wa hali ya juu, lakini wenye elimu mpya ya soka la kisasa ndiyo maana ni rahisi kwao kubadilisha baadhi ya mbinu ambazo zilikuwa zinatumika miaka kadhaa nyuma na kuleta mifumo mipya, ambayo imekuwa ikiwabeba, ila kuna wakati wanatakiwa kupewa muda ili kutimiza kile walichonacho.
Mbinu za makipa kutumia zaidi miguu kuliko mikono ni za makocha wa kisasa, zaidi wakitajwa kina Pep Guardiola ambaye alikabidhiwa timu akiwa na miaka 39 tu, lakini pia mfumo wa kuwatumia mawinga kama mabeki wa pembeni, mabeki wa pembeni kama mawinga nao ulikuwepo lakini kwa sasa ndiyo umekuwa ukitumiwa zaidi kutokana na makocha hawa kufahamu jinsi ya kuwapa majukumu vizuri, kutokana na mabadiliko ya elimu ya kila siku, lakini ndiyo jambo kubwa ambalo kwa sasa wanalisoma kwa vitendo.
Folz ni kocha kijana mwenye miaka 35, lakini jambo la ajabu ni kwamba tayari ana uzoefu wa zaidi ya miaka saba katika mabenchi ya ufundi kadhaa ambayo amepita.
Kocha huyo anayetumia mifumo ya kisasa anapenda soka la kasi, lisilo na mbwembwe nyingi, lakini anataka wachezaji ambao wanaweza kumfungia mabao mengi kwenye kila mchezo.
“Ni kocha mzuri sana kwa timu inayotaka mabao mengi, amekuwa na ubora wa juu wa kufundisha soka kwa kuwa anapenda timu inayofunga mabao mengi na haelewani na wachezaji wavuvi kwa kuwa mfumo wake unataka mchezaji aliye fiti kwa asilimia 100,” alisema Jonathan Alexandre Mtanzania aliyepo Afrika Kusini aliyemshuhudia akiwa na Mamelodi na AmaZulu .
Kocha huyo, akiwa na umri mdogo ameshafanya kazi kwenye timu 11 tofauti alianzia kuwa kocha Msaidizi, Chamois Niortais, lakini wakati anachukuliwa na Yanga alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Michezo, Olympique Akbou ya Algeria.
Lakini heshima yake kubwa ni kuwa kocha msaidizi wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, kocha mkuu, Horoya AC ya Guinea kocha mkuu, AmaZulu FC ya Afrika Kusini, kocha mkuu, Township Rollers ya Botswana.
Pia amepita kocha mkuu, Ashanti Gold Ghana, kocha kkuu, Bechem United Ghana, kocha msaidizi, Pyramids FC ya Misri Kocha Mkuu, West Virginia United ya Marekani. Pamoja na kocha msaidizi, timu ya Taifa ya Uganda.
Hata hivyo, pamoja na huyu, project ya Yanga kwenda kisasa kama zilivyo timu nyingine kubwa duniani, ilianzia pia wakati ilipomuajiri Abdihamid Mohamed Moallin ambaye ana miaka 36 pekee.
Kocha huyo anakuja na kocha wa makipa ambaye ni Majdi Mnasria raia wa Tunisia ambaye ana umri wa miaka 44 pekee, hivyo ni rahisi kusema kuwa hii ni timu ya makocha vijana kwa sasa, lakini watatakiwa kupewa ushirikiano wa kutosha.
Kwa miaka ya hivi karibuni, hii ni mara ya kwanza timu za Simba na Yanga zinaamini kwa makocha vijana wenye miaka 45 kushuka chini, kitu ambacho miaka kadhaa nyuma wasingeweza kufanya hivyo kwa kigezo kuwa hawana uzoefu, ni watoto wadogo, lakini kwa kuwa dunia imewafundisha hakuna namna tena wanalazimika kupitia njia za wakubwa wao.
Kwa upande wa Simba kelele nyingi zilipigwa wakati ilipomuajiari Fadlu Davids mwanzoni mwa msimu uliopita akiwa hana CV yoyote kubwa zaidi ya kuwa msaidizi kwenye timu kadhaa.
Fadlu naye alitua Simba akiwa na miaka 43 tu, lakini akapewa timu hiyo yenye ndoto kubwa na tayari ameshaonyesha kuwa kazi hiyo anaifahamu tena kwa kutumia wachezaji wengi vijana ambao hawana uzoefu mkubwa kwenye soka, akifanikiwa kuipeleka timu hiyo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, kitu walichokisotea kwa miaka na miaka tangu walipofika hapo kwenye Kombe la CAF mwaka 1993.
Katikati Simba ilipita na makocha wengi wakubwa na wenye wasifu mkubwa, lakini walishindwa hili ambalo Fadlu alilikamisha kwa kuwa na wachezaji wengi wachanga lakini wenye uzoefu wa juu.
Pamoja na kushindwa kutwaa kombe lolote lakini project yake inaonekana kwenda vizuri pamoja na umri wake mdogo.
Umri wa kocha huyo unaenda na kikosi chake, lakini wasaidizi wake, wa kwanza Darian Wilken ana miaka 30 tu, amezaliwa mwaka 1994, pia Riedon Berdien ana miaka 42 tu, ni kocha wa viungo wa timu hiyo, changanya na kina Seleman Matola mwenye miaka 46 na Meez Kajee, hakuna hata mmoja aliyefikisha miaka 49.
Iliwahi kuelezwa, makocha hao wamekuwa wakijifunza kila kukicha na mara kwa mara huwa na kozi kwenye kompyuta zao jambo ambalo makocha wengi wakongwe wamekuwa wakishindwa kufanya.
“Hawa jamaa wanatoa elimu kubwa sana, kwanza wanatembea na mashine yao ya kutengeneza kahawa kila mahali, wanafanya kazi hadi usiku sana ni ngumu kuwaona wakiwa wamekaa hawana kazi, kama hawafundishi basi elewa kuwa watakuwa kwenye kompyuta zao muda mwingi wakifanya kazi zao, wakisoma na wakati mwingine wamekuwa wakitazama mikanda na wapinzani na kujadiliana baadhi ya mambo,” kilisema chanzo kutoka Simba.
Jambo pekee ambalo Yanga wanatakiwa kufanya ni kupitia vizuri wasifu wa kocha huyo, siyo kocha ambaye amedumu kwenye timu moja kwa zaidi ya msimu mmoja, hivyo hilo nalo ni la kuagalia zaidi.
KWA NINI ANAFAA
Kusema Yanga imeleta kocha ambaye hana uzoefu kwenye soka hakuna hoja, kama utakuwa unakubali Mikel Arteta alienda Arsenal moja ya timu kubwa duniani akiwa anatokea kuwa msaidizi wa Pep Guardiola wa Man City akiwa hakuwahi kuifundisha timu yoyote kubwa, Arsenal walimuona wapi akifundisha zaidi ya kuwa nyuma ya Guardiola nafikiri hakuna na hata mashabiki wengi duniani walishangaa?
Lakini pia mwanzilishi wa soka la kisasa Pep raia wa Hispania hakupata mafanikio baada ya kufundisha timu kubwa bali alianza kuifundisha Barcelona akitokea kwenye timu ya vijana ya kikosi hicho La Masia akaenda timu kubwa akiwa na umri usiozidi miaka 35, kilichobaki kwa sasa ni historia na dunia nzima inatambua alichofanya.
Arteta anayesumbua kwenye soka duniani usifikiri ni mkongwe, ni mwenye miaka 42 tu na alijiunga na Arsenal akiwa na miaka 39, lakini alitengeneza benchi la ufundi la kufanana naye kama anavyofanya Fozl kwa sasa.
Manchester United ni klabu yenye ushawishi mkubwa duniani ilikuwa inaweza kumchukua kocha yeyote mwenye wasifu mkubwa, lakini kocha wake ni Ruben Amorim akitokea Ureno bila kuwa na pilika pilika nyingi za soka la ushindani tena akiwa na miaka 39 tu anaiongoza klabu hiyo.
Unaweza kuamini Liverpool inafundishwa na Arne Slots ambaye ana miaka 46 tu? Na tayari ameshaweka rekodi kadhaa kubwa zilizoshindikana kwenye kikosi hicho, kama huamini kuhusu project ya Yanga, basi waulize Liverpool walimpata wapi kocha huyo akiwa ameanza kufundisha soka kuanzia mwaka 2017 tu na tayari ameshawapa ubingwa wa Ligi Kuu England.
Hata hivyo, Bayern Munich ni mfano tosha kwa Folz, kwa sasa timu hiyo inafundishwa na Vincent Kompany ambaye aliipandisha Burnley daraja, lakini akaishusha, dunia ilishtuka baada ya Bayern kumuajiri kocha huyo akiwa na umri wa miaka 38, tayari kilichobaki kwa sasa ni historia kwenye dunia ya soka akiwa ameshatwaa ubingwa wa Bundesliga.
Kwa Afrika Mamelodi ni waumini wazuri wa makocha vijana na walichofanya kwa Rhulani Mlungisi Mokwena akiwa na miaka 33 kila mmoja alikiona na ni kocha mwenye heshima kubwa duniani.
Hakuna ubishi walichokifanya Yanga waliangalia wakubwa kwenye soka duniani wamefanya nini, tusubiri tuone kama wengine watafuata, lakini pia hawa huanza na dau dogo, mwishoni akifanikiwa klabu inabidi ufungue pochi haswa.
The post YANGA KUMPA KAZI YA UKOCHA KIJANA WA MIAKA 35 WAMEPATIA..? UKWELI UNAOPASWA KUJUA HUU HAPA… appeared first on Soka La Bongo.