Timu ya Simba inatarajia kuhamisha kambi yake huko Misri kutoka mji wa Ismailia kwenda jijini Cairo kutokana na sababu mbalimbali zilizotajwa na benchi la ufundi la timu hiyo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu kupitia tovuti ya Simba, Kocha Mkuu Fadlu Davids amesema lengo la kuhamisha kambi kwenda Cairo ni kupata mechi nzuri za kirafiki zenye ushindani.
“Tarehe 15 tutahamisha kambi kutoka Ismailia hadi Cairo, ambako tutacheza mechi za kirafiki zenye ushindani ili kujiandaa ipasavyo. Kadri tunavyocheza mechi za kirafiki, wachezaji wapya na wa zamani wanazidi kuzoeana.
“Msimu uliopita tulikuwa vizuri kwenye Ligi Kuu, lakini kwenye Kombe la Shirikisho la CAF tulikosa ubora wa kutosha. Sasa tunapanda kiwango tunakwenda Ligi ya Mabingwa Afrika, tunahitaji kikosi chenye ushindani wa hali ya juu.
“Lengo letu ni ifikapo mwisho wa kambi hii tuwe tumeshaunda kikosi kipya chenye kuelewana, kinachojua namna tunavyotaka kucheza. Tunajua aina ya wachezaji tulionao, tunajua marekebisho ya kimbinu yatakayohitajika. Tukibaki kama msimu uliopita, tutapata matokeo yale yale,” ameeleza Fadlu.
Hali ya kambi ilivyo
Katika kuelezea hali ya kambi, Fadlu amesema kwamba inawapa fursa ya kuwajua vizuri wachezaji hasa wale wageni waliosajiliwa katika dilisha hili la usajili.
“Tunafanya mazoezi mara mbili kwa siku, kuwahifadhi wachezaji kambini inatusaidia kufanikisha yote haya. Kambi inatusaidia kujua nguvu za kila mchezaji, tabia zao, na namna ya kuunda mazingira bora ya mazoezi,” amesema Fadlu.
Bado usajili unaendelea
Fadlu amethibitisha kuwa bado Simba inaendelea kufanya usajili kwa wachezaji wa ndani na wale wa Kimataifa.
“Bado kuna wachezaji wengine wanakuja kujiunga. Kuna wachezaji wa ndani na wa kimataifa wanaokuja kujiunga. Dirisha hili la usajili limekuwa zuri hadi sasa, tumefanya usajili muhimu sana,” ameeleza Fadlu.
Hadi sasa Simba imeshafanya usajili wa wachezaji wapya saba, kati yao wanne ni wa kimataifa ambao ni Rushine De Reuck, Alassane Kante, Mohamed Bajaber na Jonathan Sowah wakati wengine watatu ni Watanzania ambao ni Morice Abraham, Hussein Semfuko na Anthony Mligo.
The post FADLU ASHTUKA JAMBO ZITO SIMBA…..AWAPA MAELEKEZO MABOSI CHAP KABLA LIGI KUANZA…. appeared first on Soka La Bongo.