UDINE: MENEJA wa mabingwa wa UEFA Super Cup Paris St Germain Luis Enrique, amemwagia sifa golikipa mpya wa klabu hiyo Lucas Chevalier kwa kiwango cha kuvutia kwenye mechi yake ya kwanza kama kipa namba moja katika ushindi wao wa Super Cup dhidi ya Tottenham Hotspur.
Kipa huyo wa zamani wa Lille mwenye umri wa miaka 23 aliwekwa kwenye milingoti mitatu baada ya Luis Enrique kuweka wazi mapema wiki hii kuwa kipa mwingine Gianluigi Donnarumma ameondolewa kwenye kikosi na hivyo kumfanya mchezaji huyo wa kimataifa wa Italia kuanza kutafuta klabu mpya.
Chevalier ambaye aliwasili klabuni hapo Jumapili iliyopita alimwagiwa sifa kedekede pia kutoka kwa wachezaji wenzake pamoja na mashabiki baada ya kuokoa michomo kadhaa wa kadha ikiwa ni pamoja na mkwaju wa penalti wa Micky van de Ven.
“Tulimtegemea sana Lucas amefika tu lakini ulikuwa wakati wake wa kujionesha. Tumefurahi sana kwa sababu alifanikiwa. Hii ni PSG, lazima ujue jinsi ya kuhimili presha, Lucas ni kipa wa daraja la juu, anauwezo. Alifanya kazi yake vyema na sisi tunamkaribisha na kombe,” – alisema Luis Enrique.
Luis Enrique alitumia fursa hiyo kumpiga kijembe Donnarumma akisema alipewa ‘promo’ kubwa na vyombo vya Habari na hilo halikuwa jambo zuri kwa klabu. PSG wataanza kampeni yao ya Ligue 1 dhidi ya Nantes Jumapili.
The post “Chevalier ni golikipa wa ajabu” Enrique first appeared on SpotiLEO.