Kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’, amewaita mashabiki kujitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Mkapa, kesho Jumamosi wakati timu hiyo itakapokuwa inamalizia mechi za Kundi B dhidi ya Afrika ya Kati, huku akiahidi kuwapa raha kama alivyofanya.
Stars inakamilisha ratiba kwa kuvaana na vibonde hao wa kundi hilo, kwani imeshafuzu robo fainali mapema kwa kukusanya pointi tisa kupitia mechi tatu ilizocheza, huku wapinzani wao wakiwa wameshaanga mapema kwa kupoteza michezo mitatu iliyocheza hadi sasa.
Kufuzu kwa Stars kwenda robo fainali na kushinda mechi tatu mfululizo ni mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo kwenye michuano ya CAF tangu ilipoanza kushiriki michuano ya CAF na hata hivyo, Morocco amewahakikishia mashabiki kazi haijamalizika.
“Rekodi tuliyoiandika hatutaki kuitia doa Jumamosi (kesho) tunataka ushindi dhidi ya Afrika ya Kati ili tuendelee kuongoza kundi kama ambavyo tumejipangia tangu mwanzo wa mashindano,” alisema
“Mwanzo mzuri katika mechi tatu tulizocheza hadi sasa nafikiri ni kujitoa kwa wachezaji na kufuata maelekezo wanayopewa tuna kila sababu ya kuweka jitihada zetu kuhakikisha tunashinda mchezo ujao,”
“Mashabiki ni mchezaji wa 12, na tunapohitaji ushindi, tunahitaji sauti na uwepo wao. Tuungane kwa pamoja kuipa ushindi Stars,” alisema Morocco.