VINARA wa kundi B Tanzania kesho watakuwa kazini kwenye msako wa pointi tatu dhidi ya Afrika ya Kati mchezo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa.
Stars ina uhakika wa kucheza hatua ya robo fainali. Kwenye mechi tatu imekusanya pointi tisa ikipata ushindi kwenye mechi zote muhimu.
Ilifungua pazia Agosti 2 2025 kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso, mabao ya Sopu kwa mkwaju wa penati na Mohamed Hussen Zimbwe Jr kwa pigo la kichwa yalitosha kuwapa pointi tatu muhimu.
Kwenye mchezo huo ni kiungo Feisal Salum Fei Toto alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo na pointi tatu zilikuwa ni mali ya Tanzania. Agosti 6 ilikuwa Mauritania 0-1 Tanzania na mchezo wao uliopita ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Madagascar.
Agosti 16 itakuwa Uwanja wa Mkapa kusaka pointi tatu dhidi ya Afrika ya Kati mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa pande zote mbili.
Hemed Suleman maarufu kwa jina la Morocco amesema kuwa wapo tayari kwa mchezo na wanaamini kwamba watapata matokeo mazuri.
“Tupo tayari kwa mchezo wetu dhidi ya Afrika ya Kati, wachezaji wapo tayari kikubwa ni kufanya vizuri na kupata matokeo kwenye mchezo wetu muhimu.”