José Mourinho amefichua kwamba Lionel Messi alimfanya kuwa kocha bora, akikiri kwamba kukabiliana na Muargentina huyo mara kwa mara kulimsukuma kutafakari upya mbinu zake na kufikia kiwango cha juu zaidi cha soka.
Mtaalamu huyo wa kireno, alipambana na Messi katika baadhi ya mechi kali katika maisha yake ya soka akiwa kocha wa Inter Milan na Real Madrid.
Alipoulizwa na Sporty Net ataje mchezaji ambaye amemsaidia kukua, Mourinho alijibu: “Messi, kwa sababu kila nilipocheza dhidi yake alinilazimisha kufikiria sana.”
Wakati akiwa Inter, kikosi cha Mourinho kiliishinda Barcelona ya Messi kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2010 na baadaye akiwa Real Madrid, alikabiliana na Messi mara kwa mara katika mechi za El Clasico.
Akitafakari juu ya mechi hizo, Mourinho aliwahi kukiri kuwa uwepo wa Messi ulibadilisha njia yake ya kucheza mchezo.
“Messi hakuwahi kuichezea timu yangu, lakini alicheza dhidi yangu na amenifanya kuwa kocha bora kwasababu nilijiandaa vizuri kumzuia,” alisema José Mourinho.