DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Abdul Khamisi ‘D Voice’, ametoa wito kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), kuongeza vipengele maalum vya tuzo kwa ajili ya muziki wa Singeli, ambao umekuwa ukikua kwa kasi nchini.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, D Voice amependekeza tuzo tano mpya zitakazotambua mchango wa wasanii wa Singeli katika tasnia ya muziki.
Tuzo hizo ni: Mwandishi bora wa muziki wa singeli, tuzo kwa msanii chipukizi wa Singeli, tuzo ya wimbo bora wa ushirikiano wa singeli,, tuzo ya video bora ya Singeli kwa mwaka.
Tuzo ya heshima ya maisha yote kwa waanzilishi wa Singeli, ambapo D Voice anampendekeza Msagasumu apewe heshima hiyo kwa mchango wake mkubwa katika kukuza mdundo huo wa kipekee.
D Voice amesema kuwa hatua hii itaonesha kuthaminiwa kwa muziki wa Singeli na kutoa motisha kwa wasanii wanaojituma katika mwelekeo huo.
Ameongeza kuwa jamii ya Singeli ikiwemo wasanii na mashabiki inapaswa kutambulika rasmi kupitia tuzo hizi maalum.
Kauli hiyo imeibua mijadala mitandaoni, huku wengi wakimuunga mkono na kuona umuhimu wa Singeli kupewa nafasi yake kama utambulisho wa muziki wa kizazi kipya cha Kitanzania.
The post D Voice aomba tuzo maalum Muziki wa Singeli first appeared on SpotiLEO.