LONDON: MSHAMBULIAJI wa zamani wa mashetani wekundu Manchester United Wayne Rooney amesema kocha wao Sir Alex Ferguson asingeruhusu wachezaji wake kufanya mahojiano wakati wa mapumziko (Half-Time interviews) kama moja ya kanuni mpya za Ligi ya EPL zinavyoeleza akisema hatua ya kufanya mahojiano hayo ni ‘ujinga’.
Akizungumza kwenye podcast yake mpya kwenye kituo cha BBC, yenye jina la The Wayne Rooney Show, Rooney amesema haoni namna wachezaji wanaweza kunufaika na mahojiano ya “kijinga” yanayofanyika wakati mchezo unaendelea.
Rooney anaamini Ferguson, ambaye alikuwa bosi wake kwa miaka tisa Manchester United, angekuwa kinyume kabisa na wazo hilo kama lingetolewa wakati wa uongozi wake ingawa Mskoti huyo alifanya mahojiano ya muda wa mapumziko wakati wa mechi za Ligi ya Mabingwa.
“Najua kitu ambacho angesema na kisingekuwa kizuri, hiyo ni uhakika. Kwa hivyo hakuna namna suala hili lingetokea wakati wa Alex Ferguson” – Rooney alisema.
“Niliposajiliwa na DC United, mwanzoni walikuwa wakinitaka nifanye mahojiano wakati wa mapumziko kama mchezaji, jambo ambalo nililikataa. Nadhani lengo lako na mawazo yako kama ni mchezaji ni mechi yenyewe na nini kifanyike katika dakika 45 zijazo, utafanyaje vizuri zaidi au utaendelea kufanya vizuri kipindi cha pili.”
The post “Ferguson asingeruhusu ujinga huu” first appeared on SpotiLEO.