MTANDAONI: Zaidi ya wiki moja imepita tangu msanii maarufu wa Bongo Fleva, Raymond Shaban maarufu kama Rayvanny, aanze kushika nafasi za juu kwenye majukwaa makubwa ya muziki kidigitali kama YouTube Music na Spotify.
Mafanikio yake haya ni dalili wazi za ukuaji wake wa kasi na mvuto mkubwa aliopata katika sekta ya muziki duniani.
Kwa sasa, Rayvanny anapata wastani wa wasikilizaji wapya zaidi ya milioni 4 kila siku kwenye YouTube Music, huku kwenye Spotify akiongezea wapenzi wa muziki wake zaidi ya laki 2 kila siku. Hali hii imemfanya kufikisha jumla ya wasikilizaji milioni 50.9 kwenye YouTube Music na milioni 1.6 kwenye Spotify.
Hii ni hatua kubwa ambayo inaonesha si tu umaarufu wake, bali pia maendeleo makubwa ya muziki wa Bongo Fleva katika tasnia ya kimataifa.
Tunapoangalia mafanikio haya, ni muhimu kusherehekea jitihada za msanii huyu wa Tanzania ambaye anajikuta akipiga hatua ambazo mara nyingi tumekuwa tukiziangalia zikifanywa na wasanii wakubwa wa kimataifa.
Safari ya Rayvanny ni ishara ya matumaini kwa wasanii wa Kitanzania na muziki wa Bongo Fleva kwa ujumla, kuwa kuna nafasi ya kuvuka mipaka ya kitaifa na kufikia hadhira pana duniani.
Mafanikio haya ya Rayvanny ni sehemu ya ndoto kubwa ya kuionesha dunia kuwa muziki wa Bongo Fleva una nguvu na mvuto wa kipekee, unaoweza kutajwa kimataifa na kuibeba Tanzania katika ramani ya burudani duniani.
Safari hii ya mafanikio ni mwongozo na chachu kwa wasanii wengine wa Kitanzania kujiamini na kufanya kazi kwa bidii zaidi ili taifa letu lijivunie vipaji vyake na kusikika kwa sauti kubwa duniani.
The post Rayvanny achukua dunia Kidigitali first appeared on SpotiLEO.