“Tujaribu kuwaza kwa ukubwa baada ya Ijumaa usiku Taifa Stars kutolewa katika hatua ya robo fainali na Morocco katika michuano ya Chan. Hakukuwa na lawama kubwa kwa wachezaji wetu. Walipambana kwa kadri walivyoweza. Wanasiasa kama kawaida yao waliingilia kati kujaribu kuteka mafanikio.
.
Stars kufika robo fainali ya michuano hii unaweza kuamini ni mafanikio. Ni kweli. Kitu chochote kama ni mara ya kwanza katika mtazamo chanya basi ni mafanikio. Lakini nyuma ya pazia kuna mambo tunapaswa kufikiria kama taifa. Bado tuna safari ndefu ya MAFANIKIO ya kweli. Tuna kilomita nyingi za kuufikia ukweli.
.
Tumetumia mastaa wetu wa ndani lakini ndio hao hao ambao wanatumika katika kikosi kamili cha taifa Stars ambacho tunajivunia. Desemba wakati Wachaga wanajaa kwao kusherehekea Krismasi sisi tutakuwa Morocco kucheza Afcon na tutatumia mastaa hawa hawa.
.
Ambao wataongezeka watakuwa ni Mbwana Samatta, Simon Msuva na Novatus Dismas. Kati yao kuna uwezekano Samatta atakuwa akicheza michuano hii kwa mara ya mwisho. Hatutajua kama Msuva atakuwa na PAWA tena ya kucheza michuano hii mwaka 2027, wakati Tanzania tutakapokuwa mwenyeji tukishirikiana na wenzetu wa Uganda na Kenya.
.
Kupima uwezo wetu kama taifa katika michuano, tulipaswa kuwa katika nafasi ambazo rafiki zetu Morocco walikuwepo. Kwamba kina Achraf Hakimi hawana habari kuna timu yao inashiriki michuano kama hii. Watakapokwenda Afcon mwisho mwa mwaka sidhani kama mchezaji hata mmoja katika kikosi chao hiki cha juzi atakuwepo katika kikosi chao cha Afcon.
.
Tunakumbushana tu, safari ni ndefu kwa sababu wenzetu tumepambana nao huku wakiwa wanatuchora. Sisi tumekung’uta gunia letu kasoro Samatta, Msuva na Novatus lakini wenzetu wanaweza kuita kikosi cha wachezaji 30 bila ya kujumuisha hawa tuliocheza nao Temeke Ijumaa usiku. Na bado walitufunga na kutuondoa katika michuano.
— Legend, Edo kumwembe.