MSANII wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’, ameungana tena kimuziki na mrembo mwenye kipaji Abigail Chamungwana ‘Abigail Chams’ kwenye kazi mpya iitwayo “Lala“, wimbo ambao tayari unatikisa anga za kimataifa.
Wimbo huo umefanikiwa kufika mbali zaidi ya matarajio ya wengi, baada ya kushika nafasi ya kwanza kwenye chati za Audiomack nchini China, hatua inayodhihirisha jinsi muziki wa Bongo Fleva unavyoendelea kupenya masoko mapya duniani.
Kupitia ukurasa rasmi wa Instagram wa lebo yake, Kondegang, Harmonize aliposti picha inayoonyesha wazi wimbo wa Lala ukiongoza kwenye chati hizo, ukiwa mbele ya vibao vingine vya Bongo Fleva kama “Wewe na Mimi” wa Frida Amani na “Sale Sale” wa Geniusjini x66.
Mafanikio haya si tu kwamba yanampa Harmonize sifa kubwa kama msanii wa kimataifa, bali pia yanaongeza thamani ya muziki wa Tanzania katika jukwaa la dunia. Ushirikiano wake na Abigail Chams unaendelea kuonyesha kuwa ubunifu, ubora na ushirikiano thabiti vinaweza kuzaa matunda makubwa.
Wimbo wa Lala si wa kwanza kuwakutanisha wasanii hawa wawili, lakini kwa mafanikio haya makubwa, ni dhahiri kuwa mchemko wao wa muziki bado una nafasi kubwa ya kufanya maajabu zaidi duniani.
The post Harmonize na Abigail Chams watingisha Kimataifa na wimbo mpya ‘Lala’ first appeared on SpotiLEO.