DAR ES SALAAM:MSANII maarufu wa Bongo Fleva, Juma Mkambala almaarufu Jux, ametakiwa kufika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu shtaka la madai ya fidia ya Shilingi milioni 400, liliofunguliwa na Shaban Abdah maarufu kama Keizerpier, akidai kuwa Jux alimtumia kumwandikia nyimbo bila malipo.
Kwa mujibu wa hati ya wito wa mahakama, Jux anatakiwa kuwasilisha utetezi wake kwa maandishi kabla ya tarehe ya usikilizwaji wa shauri hilo, lililopangwa kutajwa tarehe 11 Septemba mwaka huu saa 3:30 asubuhi mbele ya Hakimu Mkazi H.A. Makube (PRM).
Mahakama imeeleza kuwa endapo msanii huyo atashindwa kuwasilisha utetezi wake kwa wakati, uamuzi unaweza kutolewa dhidi yake bila upande wake kusikilizwa.
Keizerpie amedai kuwa ndiye aliyeandika nyimbo mbalimbali zinazodaiwa kutumiwa na Jux na wasanii wengine waliomshirikisha, ikiwemo Uzuri Wako, Nitasubiri, Wivu, Nikuite Nani, You’re My, Dede ya Mimi Mars, na The Way You Are ya Vanessa Mdee – zote akiwa chini ya usimamizi wa Jux.
“Tunasubiri sasa kuona utaratibu wa mahakama ukifuata sheria na haki itendeke,” amesema Keizerpie.
Kwa upande wake, wakili wa Keizerpier, Marcello Nyilabu, amesema kuwa kabla ya kufungua kesi mahakamani walimwandikia Jux barua ya mwito ili wazungumze nje ya mahakama, lakini hakuitikia wala kujibu, hali iliyowalazimu kufungua shauri hilo.
“Mteja wangu alikuwa sehemu ya kazi ya muziki ya Jux kama mtunzi wa nyimbo, hivyo anastahili kulipwa kwa mchango wake,” amesema Wakili Marcello.
Shauri hilo linatarajiwa kuibua mjadala mpana kuhusu haki za watunzi wa nyimbo katika tasnia ya muziki nchini.
The post Jux aitwa Mahakamani kwa kesi ya fidia ya Milioni 400 first appeared on SpotiLEO.